Yanga raha sana... Hii ya Yanga haijawahi tokea
SIKIA hii, Jana Jumatano ilikuwa Aprili 8 na Yanga ilichofanya
ni kumpiga mtu mabao nane Uwanja wa Taifa. Kipigo hicho ilichotoa Yanga
kwa Coastal Union inayofundishwa na kocha mwenye maneno mengi na mikwara
ya kufa mtu, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ hakijawahi kuikumba timu yoyote ya
Bongo ndani ya miaka 10 iliyopita.
Amissi Tambwe amepiga bao tatu na kuandika ‘hat
trick’ yake ya kwanza msimu huu akimjibu Ibrahim Ajibu wa Simba
aliyekuwa pekee mwenye idadi hiyo.
Hali ikiwa hivyo kwa Yanga, mabingwa watetezi Azam
walishindwa kutamba nyumbani baada ya kung’ang’aniwa na Mbeya City na
kutoka sare ya 1-1 katika pambano jingine la ligi hiyo jana.
Yanga ilipata ushindi huo mnono na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 43 baada ya mechi 20.
Tambwe aliyefunga mabao manne, alianza kuandika
bao la kuongoza dakika ya 10 akiunganisha pasi ya kichwa ya Kpah Sherman
baada ya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na beki Oscar Joshua.
Simon Msuva alifunga bao lake la 12 katika Ligi
Kuu msimu huu baada ya kuwafunga tela mabeki wa Coastal na kuifungia
Yanga bao la pili dakika ya 24.
Wakati Coastal wakijiuliza huku wakifanya kosakosa
za hapa na pale na kupoteza nafasi za wazi, Tambwe alirudi tena kambani
kwa kufunga bao la tatu dakika ya 35 kutokana na kuunganisha shuti la
Juma Abdul. Matokeo yalikuwa mabao 3-0, Yanga wakiongoza hadi wakati wa
mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Coastal kufanya
mabadiliko ya kumtoa Rama Salim na kumuingiza Athuman Abussi, mabadiliko
ambayo hayakuwatisha Yanga kwani Tambwe alifunga bao lake la tatu
katika mechi hiyo na la nne kwa Yanga katika dakika ya 48 akimaliza pasi
nzuri ya Msuva.
Dakika ya 50 Mliberia Kpah Sherman aliondoa
‘gundu’ la miezi minne Yanga bila kufunga baada ya kuunganisha krosi ya
Tambwe na kuiandikia Yanga bao la tano. Msuva alifunga bao lake la 13
dakika za 86 akiunganisha krosi ya Tambwe na Salum Telela aliongeza la
saba la Yanga dakika ya 88 kabla ya Tambwe kufunga bao lake la nne na la
nane kwa Yanga katika pambano hilo ambalo Coastal ilifunikwa kabisa
Taifa.
YANGA: Barthez, Juma Abdul, Oscar Joshua/ Edward
Charles, Cannavaro, Yondani, Twitte/Dilunga, Telela, Niyonzima, Tambwe,
Sherman/ Nizar Khalfan na Msuva.
COASTAL: Fikirini Bakar, Juma Hamad, Mfuko
Abdallah, Chuma Yusuf, Mtama Bakar, Abdulhalim Humud, Mohammed Ally,
Yahya Ayoub, Rajab Mohammed/Sekuhe Mohammed, Bright Obinna/Mtindi
Mohammed na Rama Salum/Athuman Abussi
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, mabingwa
watetezi Azam waling’ang’aniwa na Mbeya City kwa sare ya 1-1 kwenye
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Post a Comment