Heeee... Yanga yawa gumzo Afrika nzima
KIPIGO cha mabao 8-0 ambacho Yanga iliipiga Coastal Union, kimesikika Zimbabwe mpaka Tunisia na kila mtu amepiga saluti.
Yanga ambayo kwa sasa inaonekana kuwa fiti
ilishusha kipigo hicho cha aina yake pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
bila wachezaji wake watatu wa kikosi cha kwanza.
Yanga itaongeza silaha hizo; Mrisho Ngassa, Danny
Mrwanda na Hussein Javu kesho Jumapili mbele ya Mbeya City. Kwa kawaida
jamaa hao hawanaga masihara hasa kwa wakati huu ambapo wanasaka soko nje
ya nchi huku usajili mpya ukikaribia.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ pamoja na kocha Hans Pluijm wamechekelea na kuiambia Mbeya City kwamba italijua jiji.
Kiburi hicho cha Yanga kinatokana na kwamba
kurejea kwa Coutinho kunamaliza tatizo la winga wa kushoto na kuifanya
Yanga irejee kwenye mfumo wake wa kutengeneza mashambulizi kupitia
pembeni, wakati Ngassa, Mrwanda na Javu wanaongeza wigo wa kuchagua
mastraika wa kutupia.
Lakini Yanga wanachekelea kwa vile Mbeya City
itacheza Dar na haijawahi kuifunga Yanga hivyo itakuwa inasaka ushindi
wa kwanza mbele ya Yanga ambayo iko fiti ingawa kocha Juma Mwambusi
amekomaa kwamba kitaeleweka tu hapohapo Taifa.
Yanga inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 43
baada ya kucheza mechi 20 na inafuatiwa kwa mbali na Azam yenye pointi
37 baada ya kucheza mechi 19 na Simba ni ya tatu na pointi 35 baada ya
kucheza mechi 21.
Mbeya City itakuwa na mtihani mkubwa kutafuta
ushindi wake wa kwanza dhidi ya Yanga kwani katika mechi tatu
walizocheza na washiriki hao wa Kombe la Shirikisho Afrika, imepoteza
mara mbili na mchezo mmoja ulimalizika kwa sare.
Pluijm alisema: “Tunahitaji kuweka nguvu kubwa
kama ilivyokuwa katika michezo mingine, hatutakiwi kupoteza pointi
katika dakika hizi za mwishoni japo utakuwa mchezo mgumu kuliko ule
tuliocheza Mbeya.”
Mechi nyingine kesho Jumapili itakuwa ni kati ya
Stand United na Polisi Morogoro ambapo timu zote zinapambana kujinasua
katika hatari ya kushuka daraja. Stand inashika nafasi ya 10 na pointi
24 wakati Polisi wao wanashika nafasi ya 13 na pointi 21.
JUMAMOSI
Kabla ya mechi ya Burnley na Arsenal leo Jumamosi saa 1:30 usiku, tayari mechi nne za Ligi Kuu Bara zitakuwa zimeshachezwa.
Post a Comment