UKISIKIA ujanja wa mjini ndiyo huu. Ishu ipo hivi; Yanga kupitia kwa Mwanasheria wake, Frank Chacha, ilitangaza kuishtaki Simba kwa kitendo chake cha kuingilia usajili wa Emmanuel Okwi na kutaka ilipwe fidia ya Sh1.7 bilioni.
Simba imeweka wazi kwamba wala haina tatizo na
itashiriki vizuri kutoa ushahidi wa kila kitu kuhusu madai hayo ya Yanga
na wakishinda basi wao ndiyo watadai fidia hiyo kutoka kwa Yanga.
Mabosi wa Simba wakajikausha kama hawajasikia vile
mkwara wa Yanga na kuendelea na mikakati yao ya kutwaa ubingwa wa Kombe
la Mapinduzi na walipofanikiwa wakaigeukia Yanga na kutazama madai yao.
Katika madai yake ya msingi, Yanga ilisema
itafungua kesi Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (Fifa) kudai
fidia kwa waliokuwa wachezaji wake; Okwi, Juma Kaseja na Genilson Santos
‘Jaja’ kwa kuvunja mikataba yao.
Kuhusu Okwi, Yanga inadai fidia ya Sh1.7 bilioni
kwa Simba baada ya kumtumia huku ikijua kuwa ana mkataba na klabu hiyo
ya Jangwani pia ikaihusisha timu ya Delga ya Misri ambayo ilifanya
mazungumzo na mchezaji huyo isivyo halali.
Kwa upande wake, Kaseja anadaiwa fidia ya Sh300
milioni kwa kitendo chake cha kutoonekana kazini na kuvunja mkataba
akiwa amelipwa haki zake zote wakati Jaja anadaiwa fidia ya Sh95 milioni
kwa kuvunja mkataba baada ya kushindwa kurejea nchini alipoenda
mapumzikoni kwao Brazil Novemba mwaka jana.
Baada ya kutafakari kwa kina madai hayo ya Yanga,
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema
watani wao wa jadi wanaonekana kutapatapa nje ya uwanja na watasikiliza
kesi yao ya madai na (Yanga) wakishindwa itabidi wao ndiyo walipe fidia
hiyo kwa usumbufu.
“Yanga wanadai fidia ya Sh1.7 bilioni, mbona
wanaonekana kama wanatapatapa? Nadhani wameishiwa fedha sasa, hawa
wanaonyesha ishara ya kufilisika ndiyo maana wana madai mengi yasiyo na
maana,” alisema Han Poppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la Friends of
Simba.
“Waache waende Fifa, sisi tutasikiliza madai yao
na tutatoa ushahidi wetu kuhusu kila kitu cha Okwi na Yanga wakishindwa
kesi hiyo basi wajiandae kuilipa Simba kiasi kama hicho cha fedha.”
Yaleta kocha mwingine
Siku chache baada ya kutwaa Kombe la Mapinduzi,
Simba inamleta kocha wa makipa wake na tayari ina mapendekezo ya makocha
wawili mmoja kutoka Kenya, Idd Mohamed Salim na mwingine kutoka Uganda.
Lakini kabla ya kumalizana na mmoja kati ya hao, huenda makipa wa Simba wakafundishwa kwa muda na kocha Choki Abeid kutoka Oman.
Post a Comment