Sasa Yanga imejipanga kisawasawa.. Pata habari kamili hapa





YANGA imeshinda mabao 4-0 mara mbili katika Kombe la Mapinduzi na leo Jumanne inacheza na Shaba ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan, lakini kocha wake Hans Van der Pluijm amewabeza wanaoponda ushindi wanaoupata kwa kusema hawabahatishi kwani wana kikosi imara.
Katika mchezo wake wa kwanza, Yanga iliifunga Taifa Jang’ombe inayoshiriki Ligi Daraja la Pili na kuonekana imeifunga timu dhaifu na juzi Jumapili ikaifunga Polisi ya Ligi Kuu Zanzibar kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Simba iliifunga Mafunzo ya Zanzibar bao 1-0 baada ya kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, Azam FC nayo ilitoka sare ya mabao 2-2 na KCCA ya Uganda kabla ya kuifunga KMKM ya Zanzibar bao 1-0. Katika mchezo wake wa pili Mtibwa ilitoka sare ya bao 1-1 na JKU ya Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm alisema kikosi chake hakijabahatisha hata kidogo kupata mabao manane katika mechi mbili kwani timu walizocheza nazo siyo za kubeza na zina uwezo mkubwa uwanjani, anasisitiza timu yake imefanya vizuri kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya.
“Mimi nawashangaa wanaobeza ushindi wetu na kusema tumebahatisha, hivi utabahatisha kwa mechi mbili na kushinda mabao manane? Tazama kama hawa tuliowafunga mechi ya pili (Polisi) nimeambiwa wanacheza Kombe la Shirikisho Afrika sasa ni timu nyepesi hiyo?” alihoji Pluijm.
Polisi ilishika nafasi ya pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Zanzibar na mwezi ujao itacheza na CF Mounana ya Gabon katika Kombe la Shirikisho Afrika huku KMKM bingwa mtetezi wa Zanzibar ikicheza na Al-Hilal ya Sudan katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tulicheza dhidi ya Azam watu waliona tulichofanya, tumekuja huku tukaendelea na morali ile ile ya mapambano, mbona hizo timu nyingine zinakutana na timu za hapa Zanzibar na hazishindi kama sisi?”Alihoji Pluijm.
Kocha huyo alisema kama inaonekana wanacheza na nyepesi basi na wenzao kutoka Tanzania Bara timu za Simba, Mtibwa na Azam nazo zingepata ushindi wa mabao kuanzia hata matatu, lakini hakuna iliyoweza kufanya hivyo.
Akizungumzia mchezo wa leo dhidi ya Shaba, Pluijm alisema: “Hauwezi kuwa mchezo rahisi kwani wenzetu wametusoma katika mechi zetu mbili tulizocheza sasa watakuja na mbinu za kutuzuia, lakini nitapambana kupata pointi tatu.”

No comments