Huyu ndiye anayehusika na kuondoka kwa Maximo.. Soma hapa


KAMA kuna mchezaji ambaye kocha wa zamani wa Yanga, Mbrazili Marcio Maximo hataki kulisikia jina lake basi ni Paul Ngwai wa Kagera Sugar. Ngwai ndiye aliyefunga bao pekee lililoipa ushindi wa bao 1-0 Kagera mbele ya Yanga Novemba Mosi mwaka jana kwenye Uwanja wa Kaitaba huko Kagera.
Kipigo hicho cha Yanga kilikuwa cha pili katika Ligi Kuu Bara baada ya mwanzo kufungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar. Vipigo hivi vilichangia kwa kiasi kikubwa kutimuliwa kwa Maximo kwani timu ilionekana haina uwezo wa kupambana na hata timu ambazo hazikutumia gharama kubwa kwenye usajili.
Baada ya kipigo hicho na Kagera, viongozi wa Yanga walianza kuchanganyikiwa huku wakifanya mambo yao ya chini kwa chini wakitafuta mbadala wa Maximo kwani hawakuridhishwa na uwezo wa timu kwa vipigo hivyo viwili, na timu ilipofungwa na Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe ilikuwa kama kumalizia kazi tu ya kumfukuza Maximo.
Ngwai analiambia Mwanaspoti kuwa ili mchezaji yeyote awe bora na afanikiwe kisoka ni lazima ajitunze, ajitume na ajitambue na hiyo ndiyo njia pekee anayoifanya yeye katika maisha yake ya soka.
“Binafsi najiona nipo fiti sana kwa sababu najitambua na kile ninachokifanya, najituma mazoezini na hata kuongeza mazoezi yangu binafsi bila kusimamiwa na kocha, hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kumsaidia mchezaji acheze kwa muda mrefu, siyo hilo tu ni lazima mchezaji ujitunze kwa kutofuja mwili wako,” anasema Ngwai.
Hakuna makipa, nidhamu tatizo
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linasimamia soka, kuanzia ligi kuu mpaka ligi za chini ambapo timu mbalimbali hushiriki ligi hiyo, lakini Ngwai anasema nchi hii ina makipa wengi lakini wenye vipaji ni wachache kuliko wale wanaofundishwa.
“Kuna makipa wengi wazuri nchini lakini makipa wenye vipaji ni wachache mno akiwemo Juma Kaseja, Aman Simba, Shaaban Kado, Agathon Antony na Mwadini Ally, lakini wengi waliobaki hufundishwa baada ya kuonyesha mapenzi ya kukaa golini,” anasema Ngwai.
“Nidhamu kwa mchezaji si kumwamkia ama kumnyenyekea mtu, bali ni nidhamu ya uwanjani unavyocheza na kuonyesha kiwango kizuri, kuheshimu mpira maana ndiyo ajira inayotuweka hapa tulipo. Lazima uzingatie kula na kupumzika.
“Mchezaji anayejitambua anatakiwa kujiheshimu kwa kupunguza starehe ambazo hazina tija maana ukizidisha starehe ni lazima kiwango kitashuka, starehe zipo ila zifanyike kwa kiasi kwa kuzingatia umuhimu wa kazi yako, wachezaji wengi wanapenda starehe hivyo kushindwa kujitunza na ndiyo maana hawafiki mbali katika soka,” anasema.
Wachezaji kushuka viwango
Kuna baadhi ya wachezaji inasemekana wanashuka viwango kutokana na kubadilishiwa mfumo ama fitina za viongozi lakini Ngwai anafafanua “Mchezaji mwenyewe unatakiwa kupigana kuhakikisha unapata nafasi ya kucheza, kubadilishiwa mfumo si sababu ya kushuka kwa kiwango cha mchezaji, kwasababu mchezaji unatakiwa kuwa na utayari wa kucheza nafasi yoyote ile unayopangwa.

No comments