Okwi ampagawisha Mserbia
FOWADI wa Simba ambaye mashabiki walikuwa wakimmaindi kwa madai
kwamba ni msumbufu, Emmanuel Okwi, ametua kambini kwa mbwembwe na
kufanya mambo ya maana ambayo yamemzingua na kumpagawisha kocha Mserbia,
Goran Kopunovic.
Lakini siyo hilo tu, Okwi ambaye alijiunga na
Simba akitokea Yanga amelitumia Mwanaspoti kutoa ufafanuzi wa kina kwa
mashabiki wa Simba kuhusiana na hali yake ya kuchelewa kuripoti pamoja
na mchakato wake wa harusi.
Kopunovic anayependa kufundisha vitu kwa vitendo
zaidi, alimpokea Okwi juzi Jumamosi mchana lakini katika muda mfupi
aliokaa naye akafanya mambo ambayo yalimshtua kidogo na kumfanya kocha
huyo akubali kwamba jamaa ni bonge la mchezaji tofauti na alivyokuwa
akisikia.
Kopunovic alisema amefurahishwa na kuwasili kwa
Okwi katika timu hiyo lakini kubwa lililomvutia zaidi ni vile mchezaji
huyo alivyotumia akili ya kuzaliwa kupandisha morali ya wachezaji
wenzake akiwataka kufanya kweli katika mchezo wa nusu fainali ambao
Simba iliichapa Polisi bao 1-0.
Bosi huyo alisema tofauti na alivyomtarajia, Okwi
alitumia muda mwingi kuwahamasisha wenzie kucheza kufa kupona ili awepo
katika fainali dhidi ya Mtibwa itakayopigwa kesho Jumanne usiku kwenye
Uwanja wa Amaan na kurushwa ‘Live’ na Azam TV.
Kopunovic alisema Okwi ameonyesha kitendo cha
kiungwana sana na atajaribu kukaa naye chini kujadiliana mambo ya maana
zaidi kikazi ikiwemo mbinu za kuimaliza Mtibwa Sugar ambayo imekuwa
ikiitesa Simba hivi karibuni.
“Ni mchezaji muhimu Simba, nimegundua hilo katika
muda mfupi aliokaa hapa, anajua afanye nini, angalia alivyobadilisha
morali ya wachezaji wenzake aliwapa maneno ambayo thamani yake ni
matokeo ya mechi ya nusu fainali,” alisema Kopunovic. “Nataka kufanya
kazi na wachezaji wenye akili kama hiyo, naamini mchezo ujao atakuwa
uwanjani.”
Kuhusu kuoa na ruhusa
“Nasikia tu kwamba nimekwenda kuoa mara nipo
kwenye fungate hakuna ukweli wowote mimi sijaoa bado kama inavyodaiwa,
ndoa halisi ni Julai nikitulia, hapa nilikuwa namsogeza tu mwenzangu
nyumbani,” alisema Okwi.
“Unajua kule kwetu Uganda wakati wa kuchumbia kama
nilivyofanya, ndiyo huwa muda wa hiyo sherehe fupi. Ni kama tunafanya
utambulisho tu.”
Okwi alisema aliomba muda wa kumpuzika kidogo, lakini wakati anaondoka hakuambiwa anatakiwa arudi lini.
Okwi alisema anatambua majukumu yake ndani ya
Simba ambapo alikuwa anaifuatilia timu hiyo kila hatua na sasa amerudi
rasmi kuanza kazi.
Post a Comment