Huyu ndiye aliyekuwa kiboko ya Simba.. Legendary
KATIKA toleo la Jumanne iliyopita, mshambuliaji wa zamani wa Yanga aliyekuwa kiboko ya Simba, Said Sued ‘Scud’ alizungumzia jinsi alivyoondoka katika klabu hiyo baada ya msimu mmoja wa mafanikio. Endelea…
Unaweza kushangaa kwani licha ya kufanya maajabu
kwa kuifunga Simba mara mbili katika msimu mmoja, Scud alichezea Yanga
kwa msimu huo mmoja tu, ulipomalizika alikwenda kuichezea Milambo ya
Tabora aliyodumu nayo kwa miaka mitano.
Habari zilizotawala wakati huo ni kwamba Scud
alikuwa mwenye maringo hasa baada ya kuifunga Simba mara mbili, rekodi
yake hiyo ya kuvutia ilimpa heshima ya kipekee mbele ya mashabiki wa
Yanga.
Hali hiyo ilitokana na ukweli kwamba enzi hizo
mechi za Yanga na Simba zilikuwa na mvuto wa kipekee, ilikuwa ni Simba
na Yanga hasa. Lakini Scud anasemaje kuhusu kuondoka kwake Yanga.
“Kila kitu huwa naamini ni mipango ya Mungu na siwezi kumlaumu yeyote kutokana na jambo hilo,”anasema Scud.
Scud anasema, anachokumbuka baada ya ligi
kumalizika alikwenda kwa bosi wake anamtaja kwa jina la Ramesh Patwa ili
apewe tiketi ya ndege ya kurudi kwao Kigoma.
Alipewa tiketi kama kawaida na fomu ya usajili ili
aijaze kwa ajili ya msimu ujao akaipokea, hata hivyo alishapewa
taarifa, alikuwa kwenye mpango wa kusajiliwa na kuachwa kwa kile
kilichodaiwa kuwa alikuwa na maringo.
“Nilipotoka nje nilikutana na Abbas Mchemba na
Dadi Fares wote walikuwa wachezaji wa African Sports ya Tanga na
kuniambia kuwa wanakwenda Tabora kusajili Milambo, tuliachana hapo mimi
nikaelekea nyumbani,” anasema Scud ambaye ni kaka wa kuzaliwa wa
mshambuliaji wa Coastal Union, Hussein Sued.
“Wakati huo niko na fomu yangu, lakini kumbe wale
wachezaji niliokutana nao Dadi na Mchemba walipeleka taarifa Milambo
ambayo ilimtuma mchezaji wao wa zamani Wastara Baribari anifuate Kigoma.
Tulizungumza na kukubaliana ndipo nikaenda Milambo na kusajiliwa
rasmi,”anaeleza Scud na kuwataja aliosajiliwa nao kuwa ni Jobe Ayoub,
Said John na huo ukawa mwisho wake Yanga.
Anasema, hapo alicheza misimu mitano na baada ya
hapo, alirudi kwao Kigoma na kusajiliwa na National sasa ni Mbanga FC
iliyokuwa Daraja la Pili.
Akizungumzia sababu ya kustaafu soka anasema kuwa
aliamua tu: “Sikupatwa na majeraha yoyote hadi kustaafu, niliamua
mwenyewe tu.”
Baada ya mazungumzo hayo mwandishi alimshawishi
Scud amtembeze zizini kwenye mifugo yake na kujionea kilichokuwepo, naye
bila kusita alifanya hivyo.
Post a Comment