SIMBA na Yanga zimerudi na mkwara mzito kwenye Ligi Kuu Bara ambapo zimeikejeli Mtibwa Sugar kwa kuiambia kwamba sasa ndio ngoma ya kikubwa inaanza.
Mtibwa imekaa kileleni mwa msimamo wa Ligi tangu
mwanzoni mwa msimu na imekuwa ikizitesa Simba na Yanga ambazo zimedai
kwamba zilikuwa zinausoma mchezo kwenye mechi za awali.
Timu hizo kongwe nchini ambazo zimeonekana
kuzidiwa maarifa ya uwanjani na Mtibwa, kila moja kupitia kwa makocha
wake raia wa kigeni imesisitiza kwamba sasa inafungua ukurasa mpya na
ligi ndiyo imeanza kwao, huku kiburi cha kutwaa Kombe la Mapinduzi mbele
ya Mtibwa kikiivimbisha kichwa Simba ambayo ilishinda mechi moja tu
kati ya nane za mwanzo ilizocheza kwenye ligi.
Wanachama matajiri wa Simba ambao walikuwa karibu
na timu hiyo kwenye Kombe la Mapinduzi, wamerejesha nguvu zao kwenye
Ligi Kuu na wikiendi hii wametapakaa Mtwara kuhakikisha timuj hiyo
inarejea kwenye nafasi mbili za juu kwa kuhamasisha wachezaji washinde
kwa nguvu zote.
Simba imesafiri kwenda Mtwara kucheza na Ndanda FC
ya mjini humo. Itakuwa mechi ya kwanza ya ligi kwa kocha Goran
Kopunovic aliyechukua mikoba ya Patrick Phiri mapema mwaka huu.
Yanga wao watakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kuikabili Ruvu Shooting ya Pwani, ikiwa ni mechi ya pili ya ligi kwa
Hans Pluijm aliyechukua mikoba ya Marcio Maximo mwishoni mwa mwaka jana.
Yanga v Ruvu
Yanga baada ya kutolewa mapema kwenye michuano ya
Mapinduzi iliweka kambi ya wiki nzima Bagamoyo, Pwani kujiandaa na
mchezo huo wa Ruvu ambapo kocha wa timu hiyo, Pluijm, alikuwa
akiwasisitiza wachezaji wake kuwa makini katika kufunga na kucheza kwa
kasi bila kutoa nafasi kwa adui.
Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye ligi ikiwa na pointi 14 wakati Ruvu wao wanashika nafasi ya tisa na pointi zao 11.
Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyokuwa yakiendelea
kwenye Uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya Dar, Pluijm alitumia muda
mwingi katika upigaji wa mashuti katika staili mbalimbali huku
akisisitiza mpira wa kasi na kuziba nafasi zinazoweza kutumiwa na maadui
wao.
Pluijm alisema: “Tunataka kushinda, hivyo lazima
tutumie mbinu mbalimbali, nataka timu icheze kwa kasi, lakini wasitoe
nafasi kwa adui na ndiyo maana tunaubana uwanja ndogo wakati wa mazoezi.
Ruvu wanatumia nguvu na wanakaba zaidi na kushambulia kwa kushtukiza na
ndiyo maana nataka timu icheze kwa kasi na kuziba mashambulizi yao.”
Yanga itamkosa beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’
anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu. Kiraka Mbuyu Twite naye huenda
akaukosa mchezo huo kutokana na majeraha ya goti lakini beki Rajab Zahir
tayari ameandaliwa kuziba nafasi hiyo.
Post a Comment