Alichokisema Ronaldo De Lima ni kweli? Soma hapa kujua zaidi



RIO DE JANEIRO, BRAZIL
HAKUNA kisichowezekana katika soka. Miguu bado inamuwasha Ronaldo de Lima na amedai kwamba anafikiria kurudi tena uwanjani kukipiga katika timu anayoimiliki, Fort Lauderdale Strikers, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili kule Marekani.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Jumatano, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu awe mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo, Ronaldo alisema kwamba anataka kurudi uwanjani kuisaidia timu hiyo.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 38 aliyeiwezesha Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2002, hajacheza soka tangu mwaka 2011 wakati alipoachana na klabu ya kwao Brazil, Corinthians.
Amedai kwamba anataka kurudi uwanjani akiwa mchezaji wa akiba ingawa amekiri kwamba mchakato mzima utakuwa mgumu.
“Napenda kucheza, napenda soka, soka lilikuwa maisha yangu. Ni mapenzi yangu makubwa. Nilipostaafu niliacha kwa sababu ya mwili wangu. Nilikuwa nasikia maumivu makali na nilikuwa majeruhi,” alisema Ronaldo.
“Hata hivyo kucheza soka inabidi uwe katika hali nzuri. Nitajaribu kufanya hivyo. Ni changamoto nyingine. Nina uhakika nitaisaidia ligi na nitaisaidia timu pia. Nitafanya sana mazoezi na kama kocha atanihitaji basi hauwezi kujua.
“Nitajaribu kucheza baadhi ya mechi. Mwaka huu nataka nifanye sana mazoezi. Miaka mitatu iliyopita sikufanya hivyo kwa sababu nilikuwa bize na mambo mengine. Labda kama tutafika fainali na nitakuwa najisikia vizuri kwanini nisicheze? Nitaweka jina langu katika orodha ya timu nikiwa mchezaji wa akiba.
“Nimefanya mambo mengi tofauti miaka ya karibuni. Mwaka jana nilikuwa katika Kombe la Dunia nikiwa mmoja kati ya waandaaji, pia nilikuwa nachambua mechi za michuano hiyo katika kituo cha TV cha Globo.
“Na sasa nimepata nafasi nzuri ya kuongoza timu nikiwa mmiliki. Fort Lauderdale Strikers ni timu yenye historia na utamaduni. Marekani soka linakuwa kwa hiyo nadhani ni nafasi nzuri sana.”
Ronaldo anakumbukwa kwa kufanya mambo makubwa barani Ulaya akizichezea klabu za PSV Eindhoven, Barcelona, Inter na Real Madrid. Anakumbukwa pia kwa kufunga mabao mawili murua dhidi ya kipa wa Ujerumani, Oliver Kahn, katika pambano la fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002 nchini Japan.

No comments