UONGOZI wa Yanga, umefanya uamuzi mgumu baada ya kumpiga chini
kocha wao, Marcio Maximo na kiungo Mbrazili, Emerson Rouqe (pichani)
sambamba na kumsainisha straika aliyeachwa na Simba, Amissi Tambwe.
Yanga imefikia hatua hiyo jana Jumatatu katika
dakika za mwisho za usajili wa Ligi Kuu Bara na sasa Mholanzi, Hans
Pluijm anarudi Jangwani kuziba nafasi ya Maximo akisaidiwa na Boniface
Mkwasa.
Mwanaspoti imethibisha kwamba Tambwe aliyekuwa
mfungaji bora msimu uliopita alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga
mbele mmoja wa vigogo wazito wa Jangwani, Francis Kifukwe na mwanasheria
wa klabu.
Habari za uhakika zinasema kwamba Yanga wameamua
kumtema Maximo baada ya kocha huyo kushikilia misimamo yake kwa kugoma
kumtema msaidizi wake, Leonardo Neiva ili nafasi yake ichukuliwe na
Mkwasa.
Uongozi wa Yanga ulitaka Mkwasa amuongezee nguvu
Maximo kwa maelezo kwamba timu imemzidi nguvu na anahitaji msaidizi
mzalendo lakini Maximo akagoma na kuwaambia kwamba leo Jumanne atawapa
msimamo wake ambao ni kujiuzulu.
Habari za uhakika ni kwamba Yanga wameafikiana
kumtema kiungo, Emerson ambaye usajili wake ulikuwa haujakamilika na
kubakiwa na Mbrazili, Andrey Coutinho ambaye ana mkataba mrefu.
Imeelezwa kwamba Yanga hawakubaliani na kiburi cha kocha huyo hasa kwa kumtema Hamis Kiiza na kuwabakisha Wabrazili wenzake.
Hatua hiyo ya Yanga imetokana na ushindi mdogo
inayopata timu hiyo katika mechi za hivi karibuni, usajili wa gharama
ambao hauonyeshi dalili ya kuleta matunda pamoja na kipigo cha mabao 2-0
ilichopata dhidi ya Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe.
Mabosi hao wa Yanga ambao walikutana jijini Dar es
Salaam juzi na jana wanamtaja mdachi Hans Pluijm kama mrithi wa Maximo
aliyetua nchini Juni 26, mwaka huu na kupokelewa kwa mbwembwe Uwanja wa
Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Hataki kutusikiliza kila mtu ameona kwamba
Coutinho hana uwezo wa kutosha kulingana na Kiiza tukamshauri basi kama
Kiiza hamtaki tumuondoe Coutinho ili nafasi yake tutafute mchezaji
ambaye ataisaidia timu zaidi yake lakini amekuwa hakubaliani na hilo
akisisitiza kwamba bado anamuhitaji,”alisema mmoja wa mabosi wa Yanga
ingawa aliongeza kwamba baadaye viongozi walikuja kukubaliana kwamba
abaki Coutinho na aondoke Emerson.
“Tunaachana naye ili atuachie timu yetu, kadiri
muda unavyozidi kwenda uwezo wa timu umekuwa ukipungua taratibu, Yanga
imekuwa ikishinda kwa kubahatisha sana kitu ambacho huko nyuma
hakikuwepo,”aliongeza kigogo huyo na kudai kuwa kuna kigogo mmoja mzito
ndani ya Yanga anamkingia kifua Maximo.
Katika mpango huo wa kumuondoa Maximo anayechukua
mshahara wa dola 12000 (Sh 20.8ml) kwa mwezi tayari Mwanaspoti lina
taarifa kwamba Yanga ipo katika hatua za kumrudisha Pluijm ambaye sasa
hana kazi.
Post a Comment