Kikosi cha timu ya Simba kilichoigaragaza Yanga kwenye mechi ya Mtani Jembe.
KOCHA wa Simba, Patrick Phiri amekiri kwamba straika Mliberia wa Yanga, Kpah Sherman ni bonge la mchezaji lakini akawaambia mashabiki wa Msimbazi kwamba dili zote zimetiki na safari hii wana bonge la timu ambalo halitaki suluhu ni magoli tu.
Kwa kujiamini Phiri alitamka maneno haya; “Hatuna
sababu ya kupata sare ama kupoteza mechi tena, tuna kikosi kizuri sasa
tofauti na kile cha mwanzo.”
Alisema ameamua kumsajili kiungo mshambuliaji
Simon Sserunkuma kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira na kupiga
chenga ambapo awali mshambuliaji Emmanuel Okwi pekee ndiye alikuwa
akicheza soka la aina hiyo kwenye kikosi chake.
“Naangalia pia uwezekano wa kuwaunganisha Okwi na
Danny (Sserunkuma) kwani ni mfungaji mzuri, anafahamu goli lilipo,
atatupatia matokeo pia katika mechi zetu, nafikiri kikosi changu
kimekamilika.”
Phiri aliongeza kuwa kutokana na aina ya uchezaji
ya wawili hao kufanana itakuwa ni kazi ngumu kwa mabeki wa timu pinzani
kuizuia safu yake ya ushambuliaji isifunge mabao kwani wakimkaba Okwi
basi Sserunkuma atafanikisha kikosi chake kupata matokeo.
Simba tayari imewasainisha Srerunkuma na beki Juku
Musheed na kuwaondoa kwenye kikosi chake Warundi Amissi Tambwe na
Pierre Kwizera ikiwa ni jitihada ya kuimarisha kikosi hicho
kilichokumbwa na sare mfululizo msimu huu.
“Nilikuwa na Okwi pekee kama mshambuliaji
msumbufu, aliweza kupiga chenga na kumiliki mpira kwa muda mrefu, Simon
(Sserunkuma) ni mchezaji wa aina hiyo, anajua kupiga chenga na kumiliki
mpira pia.
“Kwa sasa ninajiamini kwani akikabwa Okwi bado
nitabakiwa na mtu wa kuweza kuleta usumbufu na kutengeneza nafasi za
kufunga, ni aina ya washambuliaji niliokuwa nawahitaji kwenye kikosi
changu,” alisema Phiri.
Post a Comment