WAKATI Simba ikimsajili straika wa Gor Mahia ya Kenya, Mganda Dan Sserunkuma ambaye amechukuwa nafasi ya Mkenya Raphael Kiongera, Yanga nayo itajibu mapigo kwa kusajili straika matata kutoka Liberia anayekipiga Malaysia, lakini inafanya siri sana.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa straika huyo anayetarajia kutua nchini wakati wowote ili kumwaga wino, anaweza kuchukuwa nafasi kati ya Hamis Kiiza ambaye kiwango chake hakijaliridhisha benchi la ufundi licha ya kwamba ana mkataba wa zaidi ya miezi sita na Yanga.
Kwa mujibu wa kanuni, ili kumpisha Mliberia huyo, Yanga itapaswa kusitisha mkataba na mchezaji mwingine aliyeko kwenye usajili wao na pande zote mbili zikubaliane, lakini kinyume na hapo Yanga hairuhusiwa kusajili.
Habari za ndani zinadai kwamba benchi la ufundi limeuambia uongozi kwamba Kiiza hana manufaa kwa sasa na hata morali yake ipo chini hivyo kuendelea kubaki naye ni kufuja fedha ambazo zingesajili mashine nyingine ya maana.
Lakini mmoja wa marafiki wa Kiiza aliiambia Mwanaspoti mazoezini jana Ijumaa kwamba mchezaji huyo anaelewa kila kinachoendelea ndio maana ameamua kukaa tayari kwa lolote ingawa viongozi wa usajili wamemzuga kwamba atulize mzuka haachwi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kamati ya usajili, zinasema kwamba Maximo ameridhia mchezaji huyo asajiliwe kwa maelezo kwamba kiwango chake kiko juu ya Kiiza, lakini Mliberia huyo ambaye jina lake wanafanya siri ameiambia Yanga kwamba anataka mkataba wa mwaka mmoja na si miwili kama klabu hiyo inavyong’ang’ania.
Kwa mujibu wa viongozi mchezaji huyo amecheza misimu miwili kwenye Ligi ya Malaysia.
Usajili wa Mliberia huyo umepiga chini ujio wa straika mwingine Mzambia ambaye Maximo aliangalia maelezo yake na kuwaambia viongozi kwamba ni wa kawaida sana.
Tayari Yanga imemsajili kiungo Mbrazil Emerson de Oliviera Roque lakini wamedai kuhakikisha wanapata straika matata atakayeiwezesha Yanga kupata mabao katika mechi zao za Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani.
Emerson amechukuwa nafasi ya Geilson Santos ‘Jaja’ ambaye ameshindwa kurudi nchini alipokwenda kwao kwenye mapumziko mafupi baada ya ligi kusimama.
Hivi karibuni kulikuwepo pia taarifa za kumnasa kiraka kutoka Zambia, Jonas Sakuwaha anayekipiga TP Mazembe ambaye ilidaiwa kuamua kuachana na timu hiyo ili kwenda kujaribu changamoto mpya pamoja na straika wa AS Vital ya Uganda, Yunus Sentamu. Kwa sasa Yanga inajiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba ya Desemba 13.
Post a Comment