Kiungo wa Simba, Shaaban Kisiga afunguka
BAADA ya kutoka kifungoni, kiungo wa Simba, Shaaban Kisiga ‘Marlone’, ametoa la moyoni na kutamka kuwa anasahau yote na sasa amerudi akiwa mpya na hasira zake amezihamishia kwa Yanga katika mchezo wao wa Nani Mtani Jembe utakaochezwa Desemba 13 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Lakini amekwenda mbali na kufafanua, tukio la kusimamishwa kwake kwenye timu, analichukulia kama changamoto ya kujipanga na kujiweka tayari na lolote litakalotokea.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kisiga ambaye ni mtaalamu wa mipira ya faulo kikosini hapo alisema: “Nashukuru nimerudi kwenye timu na sasa naanza upya akili na nguvu zangu sasa ni kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe kuhakikisha tunafanya kweli. Binafsi niko vizuri, sikuwa na timu lakini nilikuwa nafanya mazoezi yangu binafsi kwa nguvu sana.
“Pia kwenye timu morali ipo juu, maandalizi mazuri na ninachowaomba mashabiki wawe na imani na kikosi chao kuwa Nani Mtani Jembe ya safari hii ni kicheko kikubwa tunahitaji sapoti yao.”
Akifafanua suala lake la kusimamishwa, Kisiga alisema: “Unajua mambo kama hayo huwa yanakuwepo nachukulia kama changamoto, pia nimejifunza kitu kuwa maisha ni kujiweka tayari na kujipanga wakati wote.”
Kisiga ni mchezaji pekee aliyerudishwa kwenye timu baada ya kusimishwa pamoja na Amri Kiemba na Haroun Chanongo kwa madai ya utovu wa nidhamu. Kiemba amenunuliwa na Azam kwa mkopo lakini Chanongo yupo mtaani akisubiri hatma yake.
Post a Comment