STRAIKA mpya wa Simba, Dan Sserunkuma, aliyeanza matizi jana Jumatatu amewaambia mashabiki wa Mnyama kuwa yeye ni mtu wa vitendo, lakini wakae mkao wa kula kwa ajili ya mechi yao ya Jumamosi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga.
Sserunkuma ambaye aliishuhudia Simba ikipigwa mabao 4-2 na Mtibwa Sugar juzi Jumapili katika mechi ya kirafiki, alisema anahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wachezaji wenzake ili wacheze kitimu, lakini ameomba video za mabeki wa Yanga.
“Napenda kufanya vitu kwa vitendo na mimi si mtu wa maneno mengi, nimekuja Simba nikiwa nimejiandaa na naamini mambo yatakwenda vizuri, kikubwa ninachohitaji ni ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu, si unajua tunacheza wachezaji 11? Viongozi na mashabiki nao washirikiane nasi,” alisema Mganda huyo aliyetokea Gor Mahia ya Kenya.
Akizungumzia kikosi cha Simba baada ya kukishuhudia dhidi ya Mtibwa ambapo yeye alikuwa jukwaani akihusisha na mechi ya Jumamosi, alisema: “Mechi itakuwa ngumu kwa namna ninavyoona, lakini tutafanya vizuri.
“ Kama nilivyosema, mbali ya juhudi zangu lakini tutafanikiwa endapo tu tutacheza kwa ushirikiano, pia maandalizi mazuri.”
Sserunkuma amesajiliwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo, lakini atakubaliwa kucheza Simba kama Raphael Kiongera wa Kenya atakubali kusitisha mkataba wake klabuni hapo kabla ya dirisha dogo halijafungwa Jumatatu.
Lakini Sserunkuma alienda mbali zaidi kwa kutaka kuona video za mabeki wa Yanga wakiwemo Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Oscar Joshua na Juma Abdul ili atengeneze mbinu za kuwakabili Jumamosi.
Alisema huwa anawasikia mabeki hao kuwa wamejenga safu hatari ya ulinzi ambayo huwa haipitiki kirahisi.
“Hawa mabeki mimi huwasikia tu kwamba kuna Cannavaro sijui na nani, lakini nataka kuwaona kwa sasa uwezo wao kwani siwezi kubaki na kumbukumbu ya uchezaji wao kwa miaka ya nyuma,” alisema.
Post a Comment