Mliberia wa Yanga atoa saa 48


Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazili Marcio Maximo 

SAA chache zijazo Yanga itamshusha nchini Mliberia, Kpah Sean Sherman, anayechezea Centikaya FC ya Cyprus na kama hiyo haitoshi ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa straika wa Mgambo, Malimi Busungu.
Endapo wachezaji hao watamalizana na Yanga ndani ya saa 48 kama ilivyopangwa, basi usajili wa Jangwani utakuwa umefungwa rasmi na kazi itabaki uwanjani.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazili Marcio Maximo, amejiridhisha na uwezo wa mchezaji huyo kutokana na dondoo zake kwenye mashindano mbalimbali ya ligi alizocheza pamoja na timu ya Taifa ya Liberia.
Sherman ambaye msimu uliopita alifunga mabao 24 kwenye Ligi Kuu Cyprus, atatua nchini kwa ajili ya vipimo na kufanyiwa majaribio ya mwisho ingawa habari za ndani zinasema ndiye chaguo la Maximo na ndio maana kocha huyo ameamua kuachana na wengine kutoka Zambia na Uganda.
Sherman alitakiwa kuwasili alfajiri ya leo Jumanne, lakini ameshindwa baada ya kudaiwa kwamba alichelewa ndege na sasa atatua keshokutwa Alhamisi alfajiri tayari kufanya yake.
Baada ya kumalizana na Yanga, mchezaji huyo atapelekwa moja kwa moja katika kambi ya Yanga iliyopo Kunduchi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba utakaochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa Hamis Kiiza ndiye aliye katika nafasi kubwa ya kuachwa ili kutimiza idadi ya wachezaji watano tu wa kigeni wanaotakiwa katika timu na atapewa kila kilicho chake kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Jumatatu ijayo.
Wageni wanaocheza Yanga hadi sasa ni Andrey Coutinho na Emerson Roque (wote wa Brazil), Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima (wote Rwanda) na Kiiza ambaye ni raia wa Uganda ambaye amekalia kuti kavu kwa kuonekana si chaguo la Maximo.
Sherman atakuwa Mliberia wa pili kucheza soka Tanzania baada ya William Fahnbullar aliyeichezea Simba mwaka 1997-1998 na baadaye kukimbilia Kajumulo World Soccer kabla ya kwenda kucheza soka Ulaya.
Hata hivyo Sherman mwenye umri wa miaka 22 na anayefanya vizuri katika kikosi cha Centikaya, ameikatalia Yanga kusaini mkataba wa miaka miwili kwa sababu zake maalumu na kukubali kusaini mwaka mmoja tu.
Endapo dili litakamilika Yanga itakuwa na mastraika watatu, wengine wakiwa ni Jerry Tegete na Hussein Javu. Kuhusu Busungu habari zinasema kwamba amefikia mahali pazuri, lakini mambo yake yanafanyika kwa siri sana na wiki iliyopita alikuwa jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na mabosi wa Yanga waliomficha kwenye hoteli moja ya Kariakoo jijini.
Bosi mmoja wa wana Jangwani hao alisema Maximo amekuwa akimfuatilia Busungu kwa kipindi kirefu baada ya kuridhishwa na kiwango chake alipomwona kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga walishinda 2-0.

No comments