Yanga ikimpata huyu kwishakazi

SIMBA kesho Jumanne inamalizana na straika namba moja kwenye Ligi Kuu Kenya, Dan Sserunkuma.
Mchezaji huyo raia wa Uganda ameibeba Gor Mahia katika mafanikio yao yote ikiwemo kutwaa ubingwa wa Kenya kwa mara mbili mfululizo ikiwemo msimu huu.
Mchezaji huyo ambaye ni mfungaji bora kwenye Ligi ya Kenya, kwake kupiga hat-trick si stori mpya kwavile ndiyo kazi yake. Makali ya mchezaji yameanza kuwastua Yanga lakini beki na kiongozi wa wachezaji wa Yanga uwanjani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amewaambia viongozi wa usajili Jangwani kwamba kuna mtu mmoja ambaye akitua Yanga biashara yote imekwisha na kelele za Sserunkuma hazitasikika.
Cannavaro ambaye amesisitiza kwamba Yanga inahitaji kusajili straika mmoja aina ya Didier Kavumbagu ambaye kazi yake ni kusumbua na kutumbukiza tu. Kavumbagu raia wa Burundi alikuwa Yanga lakini mkataba wake ulipokwisha akatua Azam.
Beki huyo amesema kiungo mpya wa Yanga, Emerson De Oliveira ameanza kuonyesha ufundi fulani katika mazoezi ya kikosi hicho lakini apewe muda huku akisisitiza kuwa kikosi chao kipo katika ubora mkubwa kwenye ulinzi na kiungo lakini mbele panahitaji kufanyiwa kazi kwa jinsi alivyoona kwenye mechi saba za ligi zilizopita.
“Emerson ameanza vizuri kuna kitu kipya amekionyesha ambacho kitafunga matatizo ya kiungo lakini sasa bado sehemu moja ambayo uongozi lazima uingalie kwa jicho la kipekee ambayo ni safu ya ushambuliaji kwa kumleta mshambuliaji mwenye kiu na ufungaji, mtu ambaye ana umahiri mkubwa kwenye kutumbukiza,” alisema Cannavaro.
“Tunao washambuliaji kama Jerry (Tegete), Kiiza (Hamis) na Javu (Hussein) lakini hawa watamuongezea nguvu huyo mshambuliaji mpya Yanga, tunahitaji mtu wa kufunga kushinda Kavumbagu ili timu itishe na kama akija mapema makali yetu yataanza hata katika mchezo ujao dhidi ya Simba itakuwa ni muhimu sana,”alisisitiza mchezaji huyo.
NIYONZIMA NAYE
AIBUKA
Haruna Niyonzima amesema alichanganyikiwa kusikia uvumi wa kifo chake siku za hivi karibuni na aliamua kukaa kimya ili jamii iamue ingawa amesisitiza kwamba wakati huu hafikirii kwenda Simba.
Lakini kuhusu mkataba wake na Yanga aliliambia Mwanaspoti: “Kweli mkataba wangu na Yanga unaelekea mwisho na sasa naweza kuzungumza na timu yoyote ile, lakini wa kwanza kuwapa nafasi hiyo ni Yanga kwani ndiyo timu ninayocheza sasa na wao ndiyo walionileta Tanzania.”
“Mpira ndiyo taaluma yangu kama Yanga wakionyesha mambo tofauti kwangu naweza kuendelea na mazungumzo na timu nyingine kwani nahitaji kucheza na kupata fedha ili maisha yangu yasonge mbele na si vinginevyo.”

No comments