Simba yashusha kifaa kingine cha Gabon

Kocha Patrick Phiri 

ACHANA na Dan Sserunkuma wa Uganda ambaye umeshamskia. Kuna mambo mawili mapya Simba.
Klabu hiyo imemshusha jijini Dar es Salaam jana Jumapili kwa siri kiungo mmoja raia wa Gabon na ilikuwa ikimalizana na straika mzalendo, Danny Mrwanda ambaye ni pendekezo la kocha Patrick Phiri.
Kama ilivyofanya siri kwa Sserunkuma, Simba ilimleta Mgaboni huyo jana mchana na ikafanya naye mazungumzo ya awali ambapo leo Jumatatu ataanza majaribio mbele ya kocha Patrick Phiri na endapo akifuzu atachukua nafasi ya Mrundi, Pierre Kwizera ambaye mkataba wake utasitishwa au atapelekwa sehemu kwa mkopo.
Mmoja wa viongozi wa Simba aliidokeza Mwanaspoti kwamba ujio wa Mgaboni huyo ni siri kubwa na wamepanga kumuonyesha leo mazoezini. Kwizera ameshindwa kuwashawishi uwanjani na hata kocha hajavutiwa na ufanisi wake.
Phiri amelithibitishia Mwanaspoti kuwa, Mrwanda ni chaguo lake katika kumaliza tatizo la ufungaji na viongozi wanafanyakazi ya kuhakikisha wananasa saini ya straika wao huyo wa zamani ambaye aliichezea Polisi Moro katika mechi saba zilizopita za ligi kuu na kufunga mabao manne moja likiwa dhidi ya Simba walipotoka sare ya bao 1-1.
Phiri alisema Mrwanda hana tofauti sana na Sserunkuma ambaye naye atasaini ndani ya saa 48 zijazo, hivyo atakuwa na uhakika wa kuwatumia mastraika wanne katika mechi zake za ligi. Mastraika wengine wa Simba ni Amissi Tambwe na Elius Maguli. “Sasa kikosi changu kinaelekea kukamilika na siwezi tena kuumiza kichwa katika nafasi ya ushambuliaji kwani nitakuwa nao wanne ambao wote wanaweza kucheza muda wowote hapo hata kama akiumia mmoja naweza kumtumia mwingine.
“Natakiwa kuwatumia wawili tu katika mechi hivyo, wengine watakuwa benchi wakisubiri kurekebisha makosa ya wenzao na watakuwa wakibadilishwa kutegemea na aina ya mechi na uwajibikaji wao mazoezini.
“Muda wowote Mrwanda atasaini kuichezea Simba, kwani muda mrefu nilikuwa namuhitaji kuniongezea nguvu kikosini na kuifanya Simba iwe na uwezo mkubwa wa kupata mabao na kutuweka katika nafasi nzuri ya kufanya vizuri,” alisema Phiri.
Kocha huyo pia alisema anaumiza kichwa kupata beki mwingine wa kati ili kuimarisha safu yake ya ulinzi ambayo inaweza kulega endapo mmoja kati ya Joseph Owino au Hassan Isihaka hatokuwepo uwanjani.
“Lazima niwe na mtu wa kuingia moja kwa moja au ambaye atatusaidia kuwa mbadala wa Owino au Isihaka. Beki huyu mpya anatakiwa kuwa na uzoefu na ligi kwani ambao hawana uzoefu tunao, ninachotaka ni kuwa na kikosi kilichotimia,” alisema Phiri raia wa Zambia.
Akizungumzia kuhusu usajili wake Simba, Mrwanda alisema: “Nimesikia hizo habari kaka na bado nipo Dar es Salaam, hakuna tatizo kama nikikubaliana na Simba nitasaini kucheza kwao.”
Wakati huohuo, mazungumzo ya usajili wa Sserunkuma raia wa Uganda anayecheza Gor Mahia ya Kenya yamefikia pazuri Simba imepanga kumtema Raphael Kiongera ili imsajili straika huyo kutimiza idadi ya wageni watano kikosini.

No comments