TAMBWE AFUNGUKA



KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm, leo Jumanne anafikisha siku ya nne tangu aanze kukinoa kikosi hicho, lakini mshambuliaji wake mpya, Amissi Tambwe, ametamka kwamba huyu ndiye kocha aliyekuwa anamuhitaji katika maisha yake ya soka.
Akizungumza na Mwanaspoti Tambwe ambaye alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili akitokea Simba, alisema amefurahia ujio wa kocha huyo ndani ya Yanga ambapo kikubwa kilichomvutia ni aina ya mazoezi ambayo hajawahi kukutana nayo katika kipindi kirefu cha kucheza soka pamoja na aina ya wachezaji.
Tambwe alisema mazoezi ya raia huyo wa Uholanzi yamejaa ufundi zaidi ambapo kila zoezi analotoa ingawa ni gumu, lakini lina uhusiano wa moja kwa moja kuweza kuwakabili wapinzani wao uwanjani jambo ambalo limemshangaza.
Alisema mara kwa mara amekuwa akikutana na makocha ambao wamekuwa wakitoa mazoezi ya mbio za kutosha hali ambayo imekuwa ikiwachosha wachezaji huku mazoezi ya mbinu yakipungua ambapo sasa anataka kuyashika vizuri mazoezi hayo ya Pluijm kuweza kuwakomesha wapinzani na kurudi katika fomu yake ya kupachika mabao.
“Kiukweli nafurahia sana ujio wa huyu kocha wakati anafika nilikuwa naogopa, unajua kila kocha mpya anapokuja mambo hubadilisha mambo, lakini huyu kocha (Pluijm) ni fundi sana mazoezi yake ni magumu wakati mnayaanza, lakini ni yale ambayo mtayatumia katika mechi,”alisema Mrundi Tambwe ambaye hana uhakika wa namba kwenye timu yake ya Taifa kutokana na kukosa mechi nyingi za kwanza za msimu huu akiwa na Simba.
“Nimefundishwa na makocha wengi lakini wengi wao wamekuwa wakihusudu sana mazoezi ya mbio nyingi ambazo kiukweli zinachosha wachezaji, kukimbia kupo lakini ni pale mnapoanza maandalizi ya mwanzo wa ligi mbali na hapo ni mazoezi ya mbinu kama anavyofanya kocha huyu.”
Tambwe pia alisifia uwezo wa straika Mliberia, Kpah Sherman.
“Kama kocha ana mpango wa kutuchezesha pamoja, basi mashabiki wa Yanga wajue watapata furaha muda wote kwani tutakuwa tumetengeneza pacha nzuri sana uwanjani,” aliongeza.
“Mwenzangu anajua kupambana na namuona atapambana vizuri na mabeki wakorofi.
“Tukizoeana tutakuwa hatari sana na jambo la kuomba kusiwepo majeruhi hapa katikati, nimemuona jamaa (Sherman) ni mzuri anajua wajibu wake uwanjani.” Tambwe ana wiki moja sasa tangu aliposajiliwa na Yanga akitokea Simba na alikuwa mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara akiwa amefunga mabao 19 akiwazidi mastraika wengine akiwamo Kipre Tchetche wa Azam FC, Elius Maguli (aliyekuwa Ruvu Shooting) na Didier Kavumbagu aliyekuwa anaichezea Yanga wakati huo.

No comments