Pluijm aanza kwa mikakati ya nguvu Yanga
KIKOSI kamili cha Yanga kimeanza mazoezi rasmi kikiwa chini ya bosi mpya wa ufundi, Mholanzi Hans Pluijm, lakini katika mazoezi hayo kocha huyo amekuwa mwiba mkali kwa wachezaji wavivu ambao hawana budi kubadilika.
Katika mazoezi ya kwanza kwa Pluijm aliyechukua nafasi ya kocha Mbrazili Marcio Maximo ‘The Chosen One’, Pluijm alianza kwa kikao kifupi kilichotumia dakika 15 ambapo kila mchezaji mpya aliyejiunga na Yanga wakati akiwa hayupo alipata nafasi ya kujitambulisha huku akimalizia kwa kuwatangazia mipango yake katika ujio wake huo wa pili klabuni hapo.
Baada ya hapo, kipa huyo wa zamani wa Uholanzi aligeukia katika ufundi wa uwanjani ambapo huko ndiko wachezaji wengi walipoanza kupata joto lake ambapo zoezi la kupiga pasi za haraka ndilo lililoonekana kuwapa shida ingawa mwisho lilianza kueleweka.
Tofauti na Maximo ambaye mazoezi yake yalikuwa yakianza saa 2:30 asubuhi na kumaliza saa 4:00, Pluijm aliwaweka katika sintofahamu wachezaji wake baada ya kuona anapitiliza wakianza kuutafuta mchana ambapo mazoezi yake aliyamaliza saa 5:15 asubuhi jambo ambalo liliwachanganya wavivu wengi.
“Nimeona wanashangaa kuhusu kuendelea na mazoezi, lakini siku zote ili upate mafanikio katika timu yako ni lazima wachezaji wawe na mazoezi ya kutosha na hili hata wanachama wa klabu wanataka kuona wachezaji wao wanakuwa fiti katika muda wote wa mchezo,”alisema Pluijm ambaye leo ataihamishia Yanga kambini mjini Bagamoyo.
Post a Comment