Simba yaahidiwa makubwa!

Kiungo mshambuliaji mpya wa Simba, Omary Mboom amesema kuwa hatofanya makosa iwapo atasajiliwa na badala yake atahakikisha anawapa raha wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kongwe nchini.
Mboom, anayetokea nchini Gambia kwenye timu ya Samger inayoshika nafasi ya nne kwenye ligi ya nchi hiyo, yupo nchini kwa ajili ya kufanya majaribio ya kujiunga na Simba ambayo inasaka mchezaji mahiri wa nafasi hiyo kusaidiana na mkongwe Shaaban Kisiga na chipukizi Abdallah Seseme.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mboom alisema kuwa amekuwa akifuatilia kwa karibu Ligi Kuu Tanzania Bara na kwa muda mrefu amekuwa akitamani kufika Tanzania, hasa baada ya kuiona Taifa Stars wakati ilipocheza na timu ya taifa ya nchi hiyo.
“Nipo hapa kwa ajili ya majaribio na nina uhakika nitafuzu na kujiunga na Simba. Natambua hiyo ni timu kubwa, inayoheshimika barani Afrika, hivyo iwapo nitafanikiwa kusajiliwa mashabiki wataiona kazi yangu,” alisema.
Aliongeza kuwa malengo yake ni kucheza soka ya kulipwa hasa barani Ulaya na ana imani kubwa Simba itamsaidia kutimiza malengo yake hasa kutokana na historia yake ya kuuza wachezaji nje pale wanapofanya vizuri na kisha kuhitajika.
Mgambia huyo ameletwa nchini na wakala wake aliyemtaja kwa jina la Gregg Keenan, raia wa Hispania. Ujio wake umewaweka kwenye wakati mgumu, Pierre Kwizera na Amisi Tambwe, raia wa Burundi.
Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema Mboom, anayetokea klabu ya Samger ya Gambia anafanya mazoezi na klabu hiyo kwa wiki mbili na iwapo kocha Patrick Phiri ataridhishwa na kiwango chake watamsajili.
Okwi, Owino waitesa Simba
Katika kile kinachoonekana Simba kuchoshwa na tabia za baadhi ya wachezaji wake kuchelewa kuripoti kambini, timu hiyo imeamua kuwa mchezaji yeyote atakayeshindwa kuripoti kambini leo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Hadi sasa, Simba inawakosa beki na nahodha wake, Joseph Owino na mshambuliaji Emmanuel Okwi, wote kutoka Uganda.
Adhabu iliyotangazwa na klabu hiyo ni kuikosa mechi ya Mtani Jembe dhidi ya Yanga, Desemba 13. Timu hiyo inaanza kambi leo Ndege Beach, nje kidogo ya jiji huku wachezaji Okwi na Owino wakiwa hawajaripoti baada ya kupewa ruhusa ya kwenda kwao, Uganda kumaliza matatizo ya kifamilia yaliyowakabili.
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola jana alionekana akimsisitiza Katibu mkuu wa klabu hiyo, Stephen Ally kuwa afanye utaratibu kuhakikisha wachezaji hao wanajiunga na wenzao leo, vinginevyo benchi la ufundi litawachukulia hatua za kinidhamu, ikiwamo kuwaondoa kwenye mechi dhidi ya Yanga.

No comments