Mapokezi ya Diamond usipime
Polisi jijini Dar es Salaam walilazimika kuingilia kati msafara wa mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya vurugu kutokea wakati mashabiki wakimlaki aliporejea nchini akitokea Afrika Kusini alikoshinda tuzo tatu za Channel O Music Video Awards.
Diamond aliyewasili saa 8:15 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiambamba na mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Sandra’ alilakiwa na mamia ya mashabiki waliowasili uwanjani hapo tangu saa 6.00 mchana.
Vikundi mbalimbali kutoka Temeke, Ilala, Kinondoni ikiwamo eneo la Tandale ambako ndiko mwanamuziki huyo alikokulia, vilifurika uwanjani hapo na mabango makubwa kuashiria ushindi wa kishindo wa mwanamuziki huyo nyota.
Hata hivyo, Diamond hakuzungumza na vyombo vya habari, kwani alipojaribu kufanya hivyo polisi waliokuwa uwanjani walimshauri aondoke eneo hilo ili kuondoa kelele, msongamano wa watu uliosimamisha shughuli katika maeneo mbalimbali alikopita.
Diamond aliondoka uwanjani hapo kwa gari maalumu na kuelekea Barabara ya Nyerere na alipofika Tazara, alishuka na kuanza kukimbia na mashabiki wake, huku akivua shati lake lililokuwa limejaa jasho. Mashabiki wake walimsindikiza mpaka Buguruni.
Maeneo ya Buguruni Malapa, barabara ilifungwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu na magari yaliyokuwa kwenye msafara na pikipiki (bodaboda) na kuwalazimisha polisi kuingilia kati na kumtaka mwanamuziki huyo aingie kwenye gari lake.
Diamond alitii na kupanda gari na msafara wake kuendelea hadi Kariakoo ambako hata hivyo fujo zilizidi kuwa kubwa huku mamia ya watu wakimsonga kwenye msafara huo.
Madereva wa bodaboda walikuwa wengi zaidi na kusababisha vurugu na zogo kubwa.
Polisi waliamuru mwanamuziki huyo anayetamba na video ya ‘Ntampata Wapi’, kuingia ndani ya gari lake, lakini haikuwezekana kutokana na mashabiki kutaka kumwona, ndipo polisi walipofungua njia ili msafara huo upite ili kuondoa msongamano.
Nyota huyo na msafara wake waliingia Barabara ya Morogoro kwa msaada wa polisi ambao walisimamisha magari yote ili msafara wa mwanamuziki huyo upite.
Baadaye walielekea Tandale, mahali alikozaliwa na kukulia mwanamuziki huyo.
Diamond alishinda tuzo tatu kupitia vipengele vya mwanamuziki bora anayechipukia, mwanamuziki bora Afrika Mashariki na video bora ya mwaka kupitia wimbo wake wa ‘My Number One’.
Post a Comment