Mwanaspoti ilipata ufafanuzi wa kiufundi kutoka kwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo Leonardo Neiva pamoja na Maximo mwenyewe wakisema kuwa kwa sasa wanafanyia kazi suala la kombinesheni ya uchezaji lakini pia kuwapa wachezaji mazoezi ambayo yatawaweka fiti.
“Tunapanga mfumo ambao utatuwezesha kutumia viungo wawili wakabaji, tuna mchezaji kama Emerson na Twite ambao wote ni wakabaji wazuri hivyo tutaweza kuwatumia wote wakati mmoja. Faida iliyopo ni kuwa Emerson anaweza kucheza kuunganisha beki na ushambuliaji pamoja na kuichezesha timu.”
Mazoezi yanayoendelea yanaonekana kutafuta mbadala wa Haruna Niyonzima kwa kumpa nafasi yake Mbrazili Emerson ambaye atakuwa akicheza sambamba na Twite pamoja na Dilunga. Safu ya ushambuliaji inatajwa kuwa na wachezaji Andrey Coutinho, Simon Msuva/Mrisho Ngassa na Jerry Tegete.
Kwa jinsi mazoezi yanavyokwenda, Niyonzima anahitaji kupambana na Mbrazili huyo pamoja na Dilunga ili kupata nafasi ya kucheza.
Neiva alisema: “Emerson ndiyo kwanza amekuja, anahitaji kuzoea mazingira ili aweze kucheza vizuri, kwa sasa bado anatengeneza pumzi na kwa hilo hatuwezi kumweka kwenye kikosi cha kwanza mpaka tuhakikishe ameendana na mfumo wa mazoezi na mazingira ya mchezo akiwa hapa Tanzania.
“Unajua Brazil anapotoka Emerson kuna joto kuliko Dar es Salaam hivi sasa, tatizo analolipata ni kuwa hali ya hewa huku Dar es Salaam ni nzito. Hivyo naamini kwa hali ilivyo atachukua muda mfupi na ataweza kuwa vizuri zaidi na kutushawishi kumwingiza kwenye timu ya kwanza.”
Kocha huyo pia amekiri kuwa straika Tegete amerithi mikoba ya Genilson Santos ‘Jaja’ ambaye aliachana na klabu hiyo mwanzoni mwa mwezi uliopita ktokana na matatizo ya kifamilia.
“Tuna mastraika wanne, yupo Kiiza (Hamis), Javu (Hussein) na Bahanuzi (Said) na Tegete lakini Tegete ni wa tofauti kwani uchezaji wake na wa Jaja hautofautiani sana ni wale wachezaji wenye kazi ya kufunga na kucheza kwenye eneo la katikati upande wa upinzani,” alisema.
“Javu ana kasi kali anapokuwa na mpira, lakini Kiiza na Bahanuzi ni wazuri wakishambulia kutoka pembeni, hivyo Tegete atakuwa mchezaji wetu wa kutegemea kwenye safu yetu ya kati.”
Kocha Neiva pia amesema kuwa wataendelea na programu yao ya mazoezi kwa wiki hii nzima kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam kisha wataweka kambi ya wiki moja kabla ya kuvaana na Simba kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe utakaopigwa Desemba 13.
Post a Comment