Hii ndiyo Simba mpya, Mtake msitake mtatupenda tu


Kiungo mpya wa Simba, Omar Mboob 

KIUNGO mpya wa Simba, Omar Mboob, ameanza majaribio ya nguvu Msimbazi lakini Makamu Rais wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ametamka kwamba kazi ya kushusha vifaa vya nguvu ndiyo kwanza inaanza na mtake msitake lazima mtaipenda Simba.
Mboob raia wa Gambia ametua Simba akitokea klabu ya Samger ya Gambia ambapo katika mazoezi ya jana Jumatatu alianzia gym ilipokuwa ikijifua timu hiyo kabla ya kuhamia kwenye mbio ndani ya Uwanja wa Sigara uliopo Temeke, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti Kaburu alisema uongozi wao ulikuwa kimya katika kuyafanyia kazi mapendekezo ya Kocha Patrick Phiri ambapo ujio wa Mboob ni sawa na kufungua njia kutokana na kwamba wapo wachezaji mastaa wengi wanakuja nyuma yake kujaribiwa Msimbazi.
Kaburu alisema Mboob ambaye anamudu sehemu ya kiungo mchezeshaji, atakuwa nchini kwa wiki mbili akifanyiwa majaribio ambapo endapo ataonyesha uwezo mkubwa atapewa mkataba ingawa hakusema ni mchezaji gani atachomolewa.
Lakini habari za ndani zinamtaja Pierre Kwizera wa Burundi kwani tayari Raphael Kiongera imebainika kwamba atampisha Dan Serunkuma ambaye leo Jumanne au kesho Jumatano atasaini mkataba na Mnyama.
“Tunataka kusuka timu yenye uwezo wa kuifunga timu yoyote, tupo katika hatua nzuri yakuleta wachezaji wengi bora, huu ujio wa Mboob ni kama kazi imeanza, hatukutaka kuongea tulikuwa kimya kwa kuwa tulikuwa katika mchakato,”alisema Kaburu.
“Kuhusu Sserunkuma tumefikia sehemu nzuri ya kumalizana naye kama mnavyofahamu amemaliza mkataba wake na Gor Mahia, lakini tupeni muda tutakayemalizana naye mtamuona hapa akiwajibika na wenzake.”
Akizungumzia hatua hiyo, Phiri alisema katika ripoti yake ya maboresho alipendekeza ujio wa kiungo mchezeshaji ambapo kwanza ataanza kwa kumuangalia Mboob huku akiwasubiri Sserunkuma, Mrwanda (Danny) na beki wa kulia na wa kati.
Wakati hali ikiwa hivyo katika usajili Phiri ameliambia Mwanaspoti kuwa kabla kikosi chake hakijaingia kambini Jumatatu wiki ijayo kujiwinda dhidi ya Yanga watakuwa na mechi mbili za kirafiki.
Phiri alisema wataumana na moja ya timu kutoka Uganda Ijumaa kabla ya kuwageukia Mtibwa Sugar watakaocheza nao siku moja kabla ya kutimkia Zanzibar katika kambi yao.

No comments