Watakaopoteza namba zao Yanga ujio wa Emerson


WACHEZAJI WA YANGA

YANGA imemsajili kiungo, Emerson Rouqe, kutoka Brazil ili kukiongezea nguvu kikosi chake kinachoshiriki Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Ujio wa kiungo huyo unatokana na Mbrazili mwingine aliyekuwa katika timu hiyo, Genilson Santos ‘Jaja’ kuamua kuachana na kikosi hicho kwa sababu alizoeleza kuwa za kifamilia zikiambatana na kushindwa kwake kuonyesha uwezo wa kuridhisha.
Akiwa na Yanga, Jaja alicheza mechi saba za awali za Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo alifunga bao moja tu.
Kocha Marcio Maximo muda mfupi tu baada ya Jaja kuamua kujiondoa Yanga, aliamua kumchukua Emerson ili kuiongezea nguvu timu yake, lakini ikiendelea kupambana na tatizo la ushambuliaji kwani atakuwa amebaki na mastraika wale wale aliowakuta wakina Hamis Kiiza, Jerry Tegete, Hussein Javu na Said Bahanuzi.
Lakini ujio wa kiungo huyo unaambatana na machungu kwa wachezaji wengine wa Yanga ambao kwa vyovyote lazima watahamishwa nafasi au kuwa katika hatari ya kupoteza nafasi tofauti na awali.
Baadhi ya wachezaji watakokuwa na wakati mgumu ni;
Mbuyu Twite
Ujio wa Emerson utasababisha kiungo mkabaji Mbuyu Twite kurejeshwa katika nafasi ya beki ya kulia alipokuwa anacheza awali na katikati akicheza Frank Domayo aliyehamia Azam. Twite akachezeshwa namba sita hadi leo. Sasa kwa kuwa Yanga ni kama imeshabariki ujio wa Emerson huku ikisisitiza kuwa itasikiliza maoni ya Maximo kama imsajili au vinginevyo huku kocha huyo akiwa ndiye aliyemleta ni wazi tayari ameshasajiliwa.
Na kama Maximo huyo huyo aliyemleta Jaja na akacheza kikosi cha kwanza basi lazima Emerson acheze, hivyo Twite ni lazima atarudishwa beki ya kulia alikozoea kucheza kabla ya ujio wa kiungo huyu raia wa Brazil. Bado Twite ataendelea kutumika kama kiraka katika kikosi cha Yanga kwani hata inapotokea mmoja kati ya mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ au Kelvin Yondani mmoja akiumua au kuwa chini ya kiwango, anawezwa kuchezeshwa kama beki wa kati.
Juma Abdul
Beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul muda wowote kuanzia sasa anaweza kurudi benchi ili kumpisha Mbuyu Twite katika nafasi hiyo kwani naye analazimika kumpisha kiungo mpya ambaye ni chaguo la kocha na hakuna wa kupinga hali hiyo.
Kabla ya msimu huu kuanza, Abdul aliyesajiliwa na Yanga kutoka Mtibwa Sugar mwaka 2012, alijihakikishia namba kikosi cha kwanza baada ya kuondoka kwa Domayo aliyejiunga na Azam FC kabla ya kuanza kwa msimu wa 2014/15 Ni wazi Abdul sasa analazimika kufanya kazi ya ziada ili ampiku Twite katika nafasi hiyo ambayo amecheza mechi nyingi katika mwaka huu kuanzia zile za kabla ya msimu na hata za Ligi Kuu Bara.
Abdul hata hivyo anaweza kupata ahueni endapo Emerson ataumia au kuonyesha uwezo mbovu uwanjani, kwani Twite atalazimika kusogezwa namba sita na Abdul atarejeshwa namba mbili kama kawaida.
Salum Telela
Kiungo Salum Telela licha ya kuwa katika ubora wake, bado hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga kwani Maximo anaonyesha kutomwamini ijapokuwa mtangulizi wake, Hans van der Pluijm alimwamin dakika za mwishoni.
Ujio wa Emerson ndiyo umezima kabisa dalili za Telela kucheza kikosi cha kwanza kwani kabla ya hapo alikuwa akitumika kama mbadala wa Juma Abdul katika nafasi ya beki wa kulia ambayo sasa anarudishwa Mbuyu Twite.
Sasa Telela atakuwa mchezaji namba tatu anayesubiri nafasi ya beki wa kulia kwani akiumia Twite atachezeshwa Abdul, hivyo nafasi yake itakuja baada ya kukosekana kw wachezaji hao wawili.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’
Unaweza ukashangaa lakini ndivyo ilivyo kwani sasa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anacheza beki ya kati akisaidiana na Kelvin Yondani lakini kwa sasa nafasi yake ipo katika hali ya hatari kwani akicheza kidogo chini ya kiwango anaweza kwenda benchi kwani Mbuyu Twite ametolewa namba sita hivyo atacheza namba mbili ambako Juma Abdul yupo vizuri hivyo anaweza kupelekwa katikati ambako anamudu kucheza endapo kuna mtu ataonekana kucheza chini ya kiwango.
Kelvin Yondani
Kama ilivyo kwa Cannavaro, Kelvin Yondani naye anaweza kuingia katika hatari ya kupoteza nafasi kutokana na ujio wa kiungo huyo Mbrazili, Mbuyu Twite anarudishwa namba mbili ambako Juma Abdul anacheza vizuri.

No comments