MBRAZIL mpya wa Yanga, Emerson Rouqe yupo Dar es Salaam lakini kabla klabu yake haijampa mkataba, Simba imefanya kweli baada ya kumaliza ubishi kwa straika mahiri wa Uganda kukubali kujiunga na klabu hiyo tayari kwa mechi za Ligi Kuu na ile ya Mtani Jembe dhidi ya Yanga Desemba 13.
Sserunkuma ambaye kocha wa Uganda, Sredejovin Milutin Micho amemtaja kama fowadi bora kwa sasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki alikuwa Dar es Salaam juzi Alhamisi ambapo alikubaliana na Simba kwamba atasaini mkataba nao Jumatano ijayo kwani mkataba wake na Gor Mahia unamalizika Jumanne.
Mchezaji huyo ameridhia kwamba atasaini mkataba wa miaka miwili na Simba na wameshakubaliana kila kitu na amefanyiwa vipimo vya afya kwa Dk Gilbert Kigadye huku wakiachana na mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Mtibwa Sugar Ame Ally na beki wa Prisons, Nurdin Chona.
Mwanaspoti inafahamu kuwa Sserunkuma aliingia nchini kwa siri kubwa na alifikia katika hoteli ya Saphire iliyopo katikati ya jiji na atatambulishwa wiki ijayo huku mechi yake ya kwanza ikiwa ni dhidi ya Yanga kwenye Nani Mtani Jembe.
Kiongozi mmoja wa Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa Sserunkuma atachukuwa nafasi ya kiungo Raphael Kiongera. Simba tayari ina wachezaji watano wa kigeni ambao ni Amissi Tambwe, Joseph Owino, Emmanuel Okwi, Kiongera na Pierre Kwizera.
Awali kulikuwepo na taarifa kwamba Kwizera anaweza kuachwa na kupelekwa kwa mkopo katika moja ya timu nchini Afrika Kusini lakini uchunguzi wa Mwanaspoti imeonekana kuwa ni vigumu mchezaji huyo kupata nafasi katika timu hiyo kwani kwa sasa hawana nafasi ya kumchukua tena.
Kwa upande wa Kiongera ambaye ni majeruhi anatarajia kupelekwa India kufanyiwa upasuaji wa goti aliloumia katika mechi yao ya kwanza ya ligi dhidi Coastal Union hivyo kumlazimu kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili na sasa kama atafanyiwa upasuaji basi atalazimika kuwa nje ya uwanja zaidi ya wiki sita ambapo anaweza kucheza mechi za ligi kuanzia Februari mwakani.
“Kila kitu kimekamilika kwa Sserunkuma, ni kama amesaini japokuwa anasubiri mkataba wake umalizike ila amekubali kuchukuwa mkataba wa miaka miwili. Amefanyiwa vipimo na daktari amethibitisha kuwa yupo safi kuichezea Simba, atatambulishwa rasmi wiki ijayo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia Hans Poppe kurejea nchini kati ya kesho (leo) Jumamosi au kesho Jumapili.”
Kuhusu usajili wa wachezaji wa ndani, kiongozi huyo alisema kwa sasa wanaangalia zaidi nafasi ya ulinzi ambayo haipo imara hivyo wameamua kuachana na Nurdin Chona ambaye amebakiza mkataba wa mwaka na timu yake pamoja na Ame.
“Sasa tunageukia kwa Salum Kimenya wa Prisons.’’
PHIRI AMSIFU SSERUNKUMA
Kocha wa Simba, Patrick Phiri ametaja sifa kuu nne anazozikubali kwa straika wao mpya Sserunkuma kuwa ni fundi wa kufunga mabao, mwepesi, imara na mzoefu katika soka ambapo straika huyo baada ya kumalizana na Simba jana Ijumaa alirudi kwao.
Post a Comment