Usajili dirisha dogo washika kasi, Yanga, Simba wadhibitiwa



LICHA ya jeuri na tambo kibao, viongozi wa Simba na Yanga wamechemka kwenye hatua za awali za usajili wa dirisha dogo baada ya kudhibitiwa kirahisi na Mbeya City na Prisons zote za Mbeya.
Simba ilikuwa ikiwania saini za wachezaji watatu ambao ni kiraka Deusi Kaseke (Mbeya City) pamoja na mabeki Nurdin Chona na Salum Kimenya (wote Prisons) kwaajili ya kujiimarisha hasa baada ya kuyumba kwenye mechi saba za kwanza za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Simba imefanya mazungumzo na wachezaji hao, lakini wakagomea dau lao kwa madai kwamba ni dogo. Hata hivyo Yanga iliposikia Simba inasuasua, kamati yake ya usajili ikaanza harakati za kumnasa Kaseke na kufanya naye mazungumzo ya awali wakamtajia dau ambalo alilipuuza akawaambia wajipange upya halafu wamfuate Mbeya watakapokuwa tayari.
Timu hizo mbili zilipanga kutuma watu mjini Mbeya wikiendi iliyopita, lakini zoezi hilo halikufanyika na wiki hii ndio mipango mingi ilipangwa kufanyika tena kwa kuviziana. Lakini Prisons na Mbeya City kwa nyakati tofauti zimekaa na wachezaji hao na kuwajaza maneno pamoja na ahadi ambazo zimefuta kabisa uwezekano wa wachezaji hao kuhamia Dar es Salaam kwa Simba na Yanga.
Meneja wa Prisons, Enock Lupyuto, amesema fedha ambazo Simba inataka kuwapa wachezaji hao ni ndogo kulinganisha na thamani yao halisi na ajira ya jeshi waliyonayo kwenye timu hiyo.
“Tumekaa chini na Chona na Kimenya na kuzungumza nao, tumewaelewesha hasara ya kwenda Simba kwa fedha ndogo ambayo wakibaki hapa kwetu wanaweza kuipata,” alisema.
“Nashukuru kwa kuwa wametuelewa na wamekubali kuachana na mipango hiyo ya kuhama kwani inaweza kuwagharimu maisha yao kwa siku za usoni, watapoteza ajira zao kwa maisha ambayo ni kamari.”
Kauli ya Lupyuto iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa timu hiyo, Oswald Morris.
Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imehakikishiwa ni kwamba wachezaji hao wawili wa Prisons wameahidiwa mikopo ya fedha na viwanja, huku Kaseke akiahidiwa kazi ya kudumu ofisini katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya inayoimiliki Mbeya City. Pia ameahidiwa mkopo wa fedha za masharti nafuu jambo ambalo limefanya wachezaji hao wote kulainika.
Simba imeongoza kwa kuzungumza na wachezaji wengi akiwemo Dan Sserunkuma wa Uganda anayekipiga katika timu ya Gor Mahia ya Kenya ambaye alisema yupo tayari kutua Simba endapo tu watampa fedha anayoihitaji na si vinginevyo.
Wengine ambao kocha Mkuu Patrick Phiri aliwapendekeza kwenye ripoti yake baada ya kumalizika kwa mechi saba za awali za ligi na kufunguliwa kwa usajili huo Novemba 15 ni wachezaji kutoka Mtibwa Sugar Ame Ally na Hamis Kessy pamoja na Danny Mrwanda wa Polisi Moro.
Chanzo cha ndani kutoka Simba kililiambia Mwanaspoti kuwa usajili unakuwa mgumu ndani ya klabu hiyo kwasababu klabu haina fedha bali wanategemea fedha kutoka kwa watu binafsi wenye mapenzi na timu katika kuhakikisha Simba inapata mafanikio.

No comments