Daktari Yanga afichua ukweli

DAKTARI wa Yanga, Juma Sufiani, amesema hali ngumu ya maisha ya nje ya uwanja, msongo wa mawazo na ugumu wa viwanja ni miongoni mwa sababu za mastaa wa soka nchini kupata majeraha ya mara kwa mara.
Daktari huyo alisema wapo baadhi ya wachezaji wanaoingia uwanjani wakiwa na mawazo mengi yanayosababishwa na hali ngumu ya maisha hivyo kukosa umakini kwenye uchezaji wao na kusababisha kuumia.
“Tatizo hali ngumu ya maisha ya Kitanzania inasababisha wachezaji kuumia, we angalia mchezaji anakwenda uwanjani akiwa na mawazo mkewe anaumwa halafu mwenyewe hana hela ya kumtibia, kwanini asiumie? Mara nyingi anakuwa hayupo mchezoni.
“Viwanja vyetu pia vinachangia majeraha haya, ni vigumu sana na havina tambarare nzuri hivyo wakati mwingine wachezaji wanajikuta wakiumia wakati wanakimbia tu uwanjani,” alisema Sufiani
“Kama ligi yetu ingekuwa ndefu kama ya England basi tungefika mwisho wa msimu kila mchezaji kaumia, ingekuwa ni aibu sana.”
Hata hivyo daktari huyo alisema kuwa hakuna haja ya wachezaji waliokwenda kwenye majukumu ya timu ya Taifa kwa kipindi hiki kupewa muda wa mapumziko kwani walikaa na timu hiyo kwa muda mfupi tofauti na kipindi cha nyuma.

No comments