Tegete aiomba Yanga ili acheze Ndondo
INAONEKANA kama uvumilivu umemshinda, kwani straika wa Yanga, Jerry Tegete ameomba viongozi wa timu za Ligi Kuu Bara kuwaruhusu wachezaji wao kucheza mechi za uswahilini maarufu kama ndondo ili kulinda vipaji vyao.
Kauli hiyo ya Tegete imekuja baada ya klabu nyingi za Ligi Kuu kuwapiga marufuku wachezaji wao kucheza ndondo kwa hofu ya kuumia na kupata mzigo wa kuwatibu wanaporejea katika timu.
Tegete alisema kwa mfano hivi sasa ligi imesimama na wachezaji wako mapumzikoni ambako hawawezi kujibweteka, wanafanya mazoezi katika timu za mitaani lakini wanapata wakati mgumu kucheza mechi kwani hawaruhusiwi na waajiri wao.
Straika huyo anafanya mazoezi binafsi kutetea nafasi yake Yanga ambayo mmoja kati ya wachezaji wanaomuweka benchi ni Genilson Santos ‘Jaja’ wa Brazil.
“Mimi naomba turuhusiwe kucheza mechi za uswahilini ili kukuza viwango kwani bila hivyo tutapoteza vipaji vyetu kwani muda wa wiki nne kukaa bila kucheza si vizuri.
“Sisi ni binadamu na huku tunapoishi kuna timu tunazofanya nazo mazoezi sasa kama umeshiriki mazoezi halafu siku ya mechi hauendi kucheza hapo hautengenezi picha nzuri kwa jamii hasa katika uhusiano, tulipaswa kusisitizwa kucheza kwa uangalifu tu,” alisema Tegete.
Mara nyingi Tegete huwa anafanya mazoezi na baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu na Daraja la Kwanza katika timu ya Tabata FC kama David Luhende wa Mtibwa Sugar, Godfrey Taita (Mwadui FC) na Ivo Mapunda wa Simba.
Kwa mujibu wa habari za ndani, mchezaji yeyote wa Yanga akithibitika kucheza ndondo anakatwa Sh400,000 katika mshahara wake.
Post a Comment