Baba ashinikiza Kiemba aondoke Simba

SHABAN Ramadhan Kiemba ‘Shundu’ ambaye ni baba mdogo wa kiungo wa Simba, Amri Kiemba, ameiomba klabu hiyo kuachana na mwanaye kuliko kukaa na kumpakazia maneno ya uongo yanayomchafua katika jamii.
Kiemba pamoja na wachezaji wengine wawili; Shaban Kisiga na Haroun Chanongo, wamesimamishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa madai ya kucheza chini ya kiwango na kuihujumu timu.
Shundu alisema: “Mwanangu (Amri Kiemba) anateseka sana na hizo tuhuma, si kweli kwamba anacheza chini ya kiwango akiwa Simba, ni mfumo ndiyo tatizo, madai wanayotoa viongozi si ya kweli kabisa.
Akiwa Taifa Stars anacheza katikati, kazi yake inakuwa kupeleka mashambulizi na kusaidia kukaba kwa wakati fulani, akiwa Simba wanamtumia pembeni, ni nafasi mbili tofauti na huwezi kutegemea ufanisi unaofanana.”
Kitaaluma Shundu ni kocha na amewahi kuzifundisha timu kadhaa nchini kama zikiwamo AFC na Palsons za Arusha, Lipuli ya Iringa na Kahama United ya Shinyanga.
“Ni bora wakamwacha tu, hajaniambia kuwa anataka kwenda wapi lakini ni bora akaenda Azam ama Yanga,” aliongeza.

No comments