Simba wajipanga kwa Kiemba, Chanongo
KATIBU Mkuu wa Simba, Stephen Ally, amesema uongozi wa klabu hiyo umepanga kumalizana na wachezaji; Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Shaban Kisiga, kabla timu hiyo haijaingia kambini Jumatatu ijayo.
Kiemba na Chanongo walisimamishwa na uongozi wa Simba kwa madai ya kucheza chini ya kiwango na kuihujumu timu hiyo wakati Kisiga alisimamishwa kwa kosa la utovu wa nidhamu baada ya kuwajibu vibaya baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ally alisema bado uongozi haujafanya maamuzi ya mwisho juu ya hatima ya wachezaji hao, lakini wamepanga kufanya hivyo kabla ya Jumatatu ambapo wachezaji wote wataingia kambini kuanza maandalizi ya mechi nyingine za ligi.
“Bado uongozi haujatoa kauli ya mwisho juu ya hatima ya wachezaji hao, bado majadiliano na vikao vinaendelea, lakini tumejipanga kulimaliza hilo kabla timu haijaingia kambini,” alisema Ally
Katibu huyo alisema mbali na sakata la wachezaji hao, uongozi wa klabu hiyo tayari umeipitia na kuipitisha ripoti ya kocha, Patrick Phiri na muda wowote kuanzia sasa watatangaza wachezaji ambao wataachwa kwenye usajili wa dirisha dogo.
Post a Comment