Okwi afunua mambo yake na Tambwe

Emmanuel Okwi.

STRAIKA aliyechukua hatamu kwenye fowadi ya Simba, Mganda Emmanuel Okwi, amesisitiza kwamba hana tofauti na mchezaji yeyote wa Simba na anatamani kucheza pamoja na mshambuliaji anayeanzia benchi, Mrundi Amissi Tambwe.
Thamani ya Tambwe ambaye alikuwa straika namba moja wa Simba msimu uliopita, imeshuka kutokana na mfumo wa kocha Mzambia Patrick Phiri ambao umemfanya aanzie benchi ingawa katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa ana nafasi kubwa ya kuanza.
Tambwe ambaye alikuwa mfungaji bora msimu uliopita, sasa anaanzia benchi na Phiri anapenda kumtumia zaidi Okwi kwa maelezo kwamba ana kasi, nguvu na anajua kutumbukiza mipira nyavuni tofauti na staili ya Tambwe ambaye ni mviziaji na akikutana na mabeki wabishi timu hukwama.
Ingawa uongozi umekanusha kwa nguvu, lakini kumekuwa na maneno kwamba thamani ya Tambwe ndani ya Simba imeshuka baada ya Okwi kutua na kwamba mchezaji huyo anafikiria kuingia mitini kwenye dirisha dogo la usajili litakaloanza Novemba 15 licha ya kwamba uongozi unajitahidi kumuweka fiti kisaikolojia.
Okwi aliyetua Simba akitokea Yanga aliyositisha nayo mkataba, alisema hana tatizo katika kucheza na Tambwe katika kikosi cha kwanza na Phiri amekiri kwamba atawapanga.
Okwi alisema anapocheza na Tambwe katika kikosi kimoja safu ya ushambuliaji yao inakuwa na makali zaidi. “Sina tatizo katika kucheza na Tambwe pale mbele wala mchezaji mwingine yeyote, nakumbuka kuna mechi tuliyocheza pamoja mimi na Tambwe tulielewana sana nikajikuta nimebanwa na mabeki lakini Tambwe akawa sehemu safi nikampa krosi akafunga kirahisi kabisa,”alisema Okwi ambaye amekuwa akijituma sana katika mechi za hivikaribuni mpaka kufikia hatua ya kucheza na majeraha.
Kwa upande wake Phiri alisema: “Kuna mechi nakumbuka walicheza pamoja Tambwe akafunga, lakini hapa kati sikuwa nawapanga pamoja kuna mambo nilikwa najaribu kuyapanga sasa Okwi anaumwa lakini akipona tutaangalia uwezekano wa kuweza kuwatumia tena kucheza pamoja katika mechi ijayo.”
Katika mazoezi ya juzi Jumatano ya kikosi hicho,  Phiri alionekana kumjaribu Tambwe katika kikosi ambacho kinaweza kuanza Jumapili huku Okwi akianza mazoezi taratibu peke yake ambapo uwezekano wa kuwepo mechi ijayo itategemea na maendeleo ya maumivu yake.

No comments