Kocha wa Azam awabadilikia wachezaji
Joseph Omog.
UKIFIKA kwenye mazoezi ya kikosi cha Azam FC, kocha wao mkuu,
Mcameroon Joseph Omog amebadilika na sasa amekuwa mkali kwa wachezaji
wake, akitaka kazi tu ifanyike na siyo masihara mengine kuhakikisha
wanafikia malengo waliyokusudia.
Omog ambaye awali alikuwa na sifa ya upole sasa ni
tofauti, ameanza na taratibu hiyo baada ya kugundua wachezaji wake
wanahitaji mchakamchaka ili kukomesha matokeo mabaya ambayo anaamini
yamesababishwa na nyota wake kudharau mechi na kutojituma.
Akizungumza na Mwanaspoti, Omog alisema: “Tatizo
kubwa la timu yangu kupata matokeo mabaya ni wachezaji kujisahau na
kudharau mechi. Ni kweli wana vipaji vya juu lakini mnapokuwa mnatafuta
ushindi lazima uongeze na vitu vingine vya ziada.
“Kipaji kinakuwapo lakini bila kujituma na kucheza
kwa moyo wa kutamani ushindi, ni ngumu kufanikiwa hivyo ninachohitaji
sasa ni mabadiliko,kikosi changu ni bora kwa sababu kinategemewa na
mataifa mbalimbali, kiufundi wako vizuri na sioni kama kuna tofauti na
Vita Club ya Congo iliyocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa wiki iliyopita
ndiyo maana nataka wajitume.”
Omog amesema, katika kuboresha kikosi chake na
kwenda sawa, anawaandaa wachezaji wake kiushindani katika kuwakumbusha
majukumu yao kila wakati ili wachangamke pia kuwajenga kisaikolojia.
Post a Comment