Niyonzima amgomea Maximo, Kaseja rasmi Simba
YANGA wanadai wameshtukia kwamba Juma Kaseja anamshawishi Haruna Niyonzima asajili Simba na tayari wamemchimba biti la uhakika ingawa kiungo huyo amesisitiza kwamba hatasaini mkataba mpya Jangwani.
Tayari, kiungo huyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine anayotaka kutokana na mkataba wake kubakiza miezi sita.
Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti Niyonzima ameeleza kushangazwa na kitendo cha kocha Marcio Maximo kumtoa kipindi cha pili bila kuambiwa sababu ili ajirekebishe. Alitolewa kwenye mechi nne mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Stand United, Kagera, Simba na Mgambo.
“Mimi ni mchezaji, ninaitumikia timu yangu ya Taifa, pia ni tegemeo katika timu hiyo, ninacheza dakika 90, sasa iweje hapa Yanga natolewa kipindi cha pili?” alihoji mchezaji huyo mzoefu.
“Kitu kingine kinachonichosha Yanga ni uzushi, ule ninaosambaziwa na baadhi ya wanachama (makomandoo) kuwa Kaseja ananishawishi nisaini Simba, kwa kuwa tunalala chumba kimoja tunapokuwa kambini,” alisema Niyonzima.
Ishu ya Kaseja
Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh amesema mchezaji huyo ni huru na anaweza kujiunga na Simba muda wowote kuanzia sasa kwani vitendo alivyofanyiwa na Yanga ni kama kuvunjiwa mkataba.
Abdulfatah aliliambia Mwanaspoti; “Ni kama Kaseja hana mkataba na Yanga kwani kila kitu kinajieleza katika mkataba wake ikiwemo kumaliziwa fedha yake na nafasi ya kucheza, sasa Yanga haijatimiza vitu vyote hivyo.
“Mteja wangu yupo huru kwani Yanga kwa kutotimiza hayo mambo wamevunja mkataba na kama kuna kiongozi wa Yanga anasema hawadaiwi na Kaseja ajitokeze, haiwezekani watu wakiuke makubaliano kienyeji.”
Kuhusu Simba kuwa na nia ya kumsajili Kaseja, Abdulfatah alisema; “Nimesikia Simba wanamtaka Kaseja, hiyo haina tatizo kwani wameonyesha nia ya kumchukua kwa sababu wanafahamu kuhusu uwezo wake waje tuzungumze tufanye biashara.” Lakini Mwanaspoti linajua kwamba kipa huyo ameshafanya mazungumzo na kumalizana na Simba na kuanzia Januari atakuwa kwenye uzi wa Simba.
Tangu aliposajiliwa na Yanga Novemba mwaka jana, Kaseja ameshindwa kupata nafasi kikosi cha kwanza na kutoa nafasi kwa Deo Munishi ‘Dida’ katika mechi nyingi za Ligi Kuu Bara hata za kirafiki
Post a Comment