Mbio za urais 2015 zaipasua UVCCM

Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Sadifa Juma Khamis
Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Sadifa Juma Khamis










MAKUNDI ya urais yanadaiwa kuugawa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), ambapo imeelezwa kuwa baraza kuu la umoja huo, limegoma kupitisha jina la Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa Naibu Kamanda wa umoja huo upande wa Tanzania Bara.
Hayo yamejitokeza katika vikao vya baraza kuu la umoja huo ambalo lilikuwa na vikao vyake mjini hapa kuanzia Novemba 7, 2014 na kuhitimishwa jana.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wakati wa vikao vya baraza hilo chini ya mwenyekiti wa UVCCM taifa, Sadifa Juma Khamis, wajumbe walikataa kupitisha jina la Pinda huku viongozi wa juu wakidaiwa kuhusika na rushwa ili kusuka mpango huo.
Akizungumzia suala hilo,  Sadifa alisema katika uteuzi wake hakupendekeza jina la Pinda kuingia katika kikao hicho ila aliliomba Baraza Kuu limpe muda ili jina la mtu kutoka bara liletwe katika kikao kijacho.
“Ni kweli niliitisha kikao cha Baraza la Utekelezaji,  baada ya kushauriana na wenzangu tuliona jina la Balozi Seif halina tatizo na Kamanda Mkuu, Mzee Kingunge (Ngombale), kwa upande wa Bara tumekubaliana jina lije kikao kijacho si sasa,” alisema.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kiliambia MTANZANIA kuwa hoja ya kupitishwa kwa Kamanda Mkuu wa UVCCM ilikuwa nyepesi hivyo wajumbe kwa kauli moja waliridhia kupitishwa kwa mwanasiasa mkongwe , Kingunge Ngombale Mwiru kuchukua mikoba  iliyoachwa na waziri mkuu wa zamani, marehemu Rashid Mfaume Kawawa.
Chanzo hicho kilisema kuwa mpango wa uteuzi wa Pinda kuwa Naibu Kamanda ulikuwa ukiratibiwa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda na Katibu wa Uchumi wa umoja huo, Omari Suleiman.
Chanzo hicho cha habari kilisema katika kikao hicho wajumbe walikuwa wakali na hata kumwambia mwenyekiti, katibu mkuu pamoja na mchumi warudishe Sh milioni 50 walizopewa kukamilisha mpango huo.
“Juu ya tuhuma kuwa tumepewa na Pinda Sh milioni 50 si kweli, fedha hizo zimetoka kwa Rais Kikwete na Kinana (Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana), ambaye naye aliwasiliana na Ridhiwani (Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze), na yeye alimpa mtu mwingine.
“Baada ya huyo mtu kupewa fedha hizo  na Ridhiwani, ilibidi tumuombee lifti kwenye ndege ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa anakuja Dodoma, tulifanya hivyo kutokana na uharaka wa kuzihitaji fedha hizo na usalama pia, sasa hiyo ni dhambi?,” alihoji Sadifa.
Kwa upande wake,  Mapunda alipuuza madai hayo na kueleza kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.
Alisema jambo la msingi lililokuwa likiwakabili ni kuhakikisha kuwa ni kikao hicho kufanyika kwa amani na salama bila watu kupigana.
“Hapa hali ni shwari maana kikao kilikuwa na hofu kubwa ya kuvurugika na baada ya watu kuona mambo yao yamekwama, wamehamia kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Mapunda

No comments