Matajiri Yanga wasaka straika

Kocha wa Yanga, Marcio Maximo
YANGA ina mastraika watano, lakini kamati yake ya usajili imeagizwa kusaka fowadi mwenye vitu kama vya Mkenya Boniface Ambani ambaye aliichezea Yanga msimu wa 2008/9 na kupachika mabao 18.
Ambani anakumbukwa na Yanga kwa kutoa pasi nzuri kwa Mkenya mwenzake, Ben Mwalala aliyepachika bao pekee la Jangwani lililofuta uteja wa Yanga kwa Simba ndani ya Uwanja wa Taifa jijiji Dar es Salaam wakati huo.
Kocha wa Yanga, Marcio Maximo, ambaye anatua nchini leo Alhamisi kutoka kwao Brazil, amewaambia mabosi wake kwamba anataka straika msumbufu kwa mabeki, mwenye nguvu na uwezo wa kutupia sekunde yoyote ile.
Mmoja wa wajumbe muhimu kwenye kamati ya usajili wa Yanga, Isaack Chanji, aliiambia Mwanaspoti jana kwamba kocha huyo amewapa uhuru wamsajili straika huyo kutoka popote ili mradi awe na vigezo hivyo alivyowapa.
“Tunasaka straika mithili ya yule Ambani (Boniface) au Mwape (Davies) mwenye nguvu na akili ya kufunga, tukishampata huyo na kocha akajiridhisha tutajua cha kufanya kuanzia hapo,” alisisitiza bosi huyo.
“Leo Yanga ina wachezaji ambao wanakaa jukwaani wakati wenzao wakiwa uwanjani, hawatumiki na mpaka sasa hawajacheza hata mechi moja, hiyo ni hasara, hatutaki kuingia huko tena, tutafanya masuala ya usajili kwa matakwa na ubora wa hali ya juu,” alisema.
Ambani ambaye ni Mkenya na Mwape raia wa Zambia waling’ara na Yanga kutokana na uzoefu waliokuwa nao, nguvu na maumbo makubwa, nidhamu ya mazoezi pamoja na uwezo mkubwa wa kupachika mabao kwenye mazingira magumu jambo ambalo limekuwa likiwashinda wengi kwa sasa.
Ingawa Chanji hakupenda kufafanua lakini endapo straika huyo akipatikana huenda mmoja wa wachezaji wawili wa kigeni ambao ni Hamis Kiiza wa Uganda na Geilson Santos ‘Jaja’ wa Brazil akaonyeshwa mlango wa kutokea.
Habari za ndani zinadai kwamba benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi hawajaridhishwa na ufanisi wa wachezaji hao haswa ukizingatia kwamba Yanga inajiandaa kwa Kombe la Shirikisho mwakani ambako imepania kupiga hatua zaidi ya miaka iliyopita.
Kuhusiana na Hamis Kiiza, Chanji alisema kuwa mchezaji huyo amebakiza miezi sita na hawawezi kusema kama watamsajili au kumuacha kutokana na mahitaji ya timu kutojulikana.
“Kama nilivyosema, Kiiza bado ni mchezaji wetu na endapo tutapata mbadala zaidi yake, hatutakuwa na jinsi, tutaachana naye, lakini kwa sasa ni mapema sana,” alisema.

No comments