Chanzo cha ugomvi wa Ndumbaro na Malinzi hiki hapa
Mwanasheria Damas Ndumbaro
NYUMA ya moshi mkubwa unaoutazama kwa mbali, chini yake kuna moto. Si kila mmoja anaweza kuuona moto, lakini wote tunaweza kuuona moshi hata tukiwa tumesimama kilomita mbili kutoka tuliposimama.
Mwanasheria Damas Ndumbaro ambaye kwa wiki kadhaa
sasa amekuwa katika mkwaruzano mkubwa na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), anafichua kwa kina kile ambacho kimejificha katika mgogoro wake
na shirikisho hilo.
Basi la Taifa Stars, Urais TFF vyahusishwa
“Kuna mambo mengi ambayo yamejificha nyuma ya
mgogoro huu, lakini nadhani chuki yangu na bwana Malinzi imechangiwa na
mambo matatu,” anasema Ndumbaro kwa kujiamini katika mazungumzo
aliyofanya na Mwanaspoti.
“Sababu ya kwanza ni pale lilipokamatwa basi la
TFF kwa deni ambalo nadhani linazidi Shilingi 150 milioni. Malinzi
alimpigia simu Silas Mwakibinga (Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi) akimwagiza
kwamba Bodi ya Ligi itoe pesa hizo kwa ajili ya kukomboa basi hilo,”
anasema Ndumbaro.
“Mimi niligoma kwa sababu ni mmoja kati ya watu
waliokuwa wanatia saini katika utokaji wa pesa hizo. Pesa ambazo
zilikuwepo pale ni za Yanga. Unajua mpaka leo Yanga hawajafika kuchukua
pesa zao ambazo zipo katika udhamini wa Azam TV na sisi bado
tumewawekea. Nikamuuliza Mwakibinga, hawa Yanga kuna mtu mmoja tu
anaweka ngumu pale, lakini vipi kama akiondoka ghafla leo? Kesho asubuhi
tu watakuja kuzichukua. Nikagoma.” “Mwakibinga alimwambia Malinzi
aongee na mimi lakini akagoma, akasema ‘Mimi siwezi kuongea na
Ndumbaro.”
Ndumbaro anadai kwamba sababu ya pili ilikuwa ni pale alipokataa wakaguzi waliochaguliwa na Malinzi wasiikague Bodi ya Ligi.
“Nadhani wakati anaanza kututafuta sisi watu wa
Bodi ya Ligi akiamini kuwa labda tuna pesa nyingi sana akatuma wakaguzi
wake waje kutukagua. Aliituma kampuni ya Price Waterhouse Coopers.
Wakaja jamaa fulani pale wawili ni Wahaya, nikajua dhumuni lao lilikuwa
nini,” anasema Ndumbaro.
“Lakini kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wakaguzi wa
TFF pekee ndio wanaoruhusiwa kutukagua sisi Bodi wa Ligi. Hapo Malinzi
alikuwa anakaribia kuvunja katiba. Nikaona bora nimuokoe kwa kugomea
wale wakaguzi wake. Alipouliza kutoka kwa wapambe wake akaambiwa
Ndumbaro ndiye amezuia. Akaweka kinyongo.”
Baada ya sababu hizo mbili, Ndumbaro anaamini kuwa
sababu ya tatu kubwa zaidi ambayo ni ya msingi ni jinsi ambavyo Malinzi
amedanganywa na wapambe wake kuwa nautaka urais katika uchaguzi ujao.
“Wapambe wa Malinzi wamemdanganya kuwa Friend’s of
Simba wanamuandaa Ndumbaro kuwa rais mpya wa TFF mara Malinzi
atakapomaliza kipindi chake cha kwanza kitu ambacho siyo kweli. Napenda
nikutamkie, mimi sina ndoto hizo. sina mpango huo kabisa na Malinzi
aelewe hivyo. Kifungo chake cha miaka saba kimelenga kuhakikisha kuwa
anamaliza vipindi vyake vyote viwili kwa amani kabisa,” anasema
Ndumbaro.
“Baada ya hayo mambo yake mawili hapo juu kukwama
ndio akataka kuvunja Bodi ya Ligi. Kumbe katiba ilikuwa inambana. Ndio
maana mpaka leo unasikia kimya.”
Post a Comment