Umegombana na mwenza wako? Fuata njia hizi kurudisha upendo wenu

Kugombana ni jambo ambalo halikwepeki
katika uhusiano wa kimapenzi . Upo ugomvi
ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi
lakini upo ugomvi ambao huwa mkubwa na
kama ukitokea na ukashindwa kujua nini cha
kufanya kuweka mambo sawa , husababisha
ufa kwenye penzi lenu .
Leo tutazungumzia mambo muhimu ya
kufanya inapotokea wewe na mpenzi wako
mmeingia katika ugomvi mkubwa,
mmetoleana maneno machafu au hata
kupigana.
1. TAFAKARI CHANZO CHA TATIZO
Kuna usemi kwamba ukitaka kulitatua vizuri
tatizo ni lazima kwanza ujue chanzo cha
tatizo lenyewe . Ukishindwa kugundua chanzo
cha tatizo, basi na wewe unakuwa sehemu
ya tatizo .
Utashangaa kwamba wapenzi wengi
hugombana na mambo kuwa makubwa
kabisa kwa sababu ya vyanzo vidogo
ambavyo walishindwa kuvigundua mapema
na matokeo yake vikazaa matatizo mengine.
Mfano rahisi , chanzo kinaweza kuwa mpenzi
wako amekupigia simu lakini ukashindwa
kuipokea kwa muda muafaka . Atakapopiga
kwa mara nyingine au mkikutana , usitegemee
atakufurahia kwa sababu atahisi
umemdharau kwa kutopokea simu
yake. Endapo ukifanya makosa ya kushindwa
kuliona kosa lako mapema na kushindwa
kuomba radhi au kutoa maelezo
yanayoeleweka kwa nini hukupokea simu,
matokeo yake utamjibu vibaya , naye
atakujibu vibaya na mwisho mtaishia
kupigana au kuachana kabisa mkiwa
mmeshatoka kabisa kwenye kosa la msingi .
Bila shaka msomaji wangu umeona jinsi
chanzo kidogo kinavyoweza kusababisha
tatizo kuwa kubwa . Ndoa nyingi au uhusiano
unaofika mwisho huwa umesababishwa na
mambo madogo ambayo yalishindwa
kutafutiwa suluhu mapema .
Katika kila ugomvi unaotokea , jambo la
kwanza jipe muda wa kutafakari chanzo
kilichosababisha mkagombana. Wakati
mwingine wewe ndiyo unaweza kuwa chanzo
cha tatizo lakini kama ukiyajua makosa yako
mapema na kukiri kisha kuomba radhi kwa
mwenzio , utakuwa kwenye nafasi nzuri ya
kurudisha mapenzi kwa haraka .
2. MPE MUDA HASIRA ZIISHE
Kila binadamu ameumbwa akiwa na hasira
na kwa bahati mbaya ni wachache
wanaoweza kuzidhibiti hasira zao. Ni rahisi
mtu kutukana , kupiga au kuharibu vitu akiwa
na hasira . Baada ya kugombana, kila mmoja
lazima atakuwa na hasira na njia pekee
inayoweza kuepusha matatizo zaidi , ni kujipa
muda na kumpa muda mwenzako ili hasira
zipungue.
Kama mpo sebuleni na umetokea ugomvi, ni
busara kwenda chumbani au nje mpaka
hasira zako zikiisha. Ni makosa kulazimisha
suluhu wakati kila mmoja akiwa na jazba
kwani mtaishia pabaya zaidi .
Ukishaona hasira zako zimetulia na
mwenzako naye ametulia , unaweza
kuanzisha mada juu ya kilichosababisha
mkagombana. Tumia lugha ya upole kwani
endapo utakuwa ukifoka au kuzungumza kwa
sauti ya juu, matokeo yake mtarudia tena
kugombana.
3. MPE NAFASI YA KUZUNGUMZA
Huwezi kumuelewa mtu kabla hujampa nafasi
ya kuzungumza na kumaliza kile
alichokusudia kukisema . Endapo tatizo
limetokea na upo kwenye hatua za kusaka
suluhu, mpe mwenzako nafasi ya kueleza
dukuduku lililopo ndani ya moyo wake.
Usimkatishe wala kumbishia chochote,
muache aongee ulichomuudhi mpaka
dukuduku lake liishe kisha na wewe jieleze
kwa upole na sauti tulivu .
4. OMBA MSAMAHA
Hakuna silaha nzuri inayoweza kukusaidia
kuushinda ugomvi wowote na kutuliza
mambo kabla hayajawa mabaya kama
kuomba msamaha. Neno ‘ samahani ’ ni dogo
lakini lina maana kubwa kwa yule mtu
anayelitoa na anayelipokea.
Hata kama unaona dhahiri kwamba kosa siyo
lako , omba msamaha kwanza kisha baada ya
hapo anza kumuelewesha mpenzi wako kwa
upole. Lazima mwisho na yeye atayaona
makosa yake na kukuomba msamaha,
mtaweza kuepuka kuukuza ugomvi huo na
kurudisha hisia za mapenzi .
5. USIWEKE KINYONGO
Endapo umeamua kuomba msamaha kwa
mpenzi wako , au yeye amekuomba msamaha,
samehe kwa dhati kutoka ndani ya moyo
wako na sahau kile kilichotokea . Ni kosa
kubwa kuweka kinyongo rohoni, yaani
unamwambia kwamba umemsamehe wakati
moyo wako bado una hasira naye .
Ukisamehe kwa dhati , jifunze na kusahau
kwani kusamehe kunaenda sambamba na
kusahau.
Wazungu wanasema forgive and forget .
Elewa kwamba mpenzi wako ni binadamu
ambaye hajakamilika, wala si malaika.
Lazima atakuwa akikosea mara kwa mara,
endapo utakuwa ukilimbikiza vinyongo,
unafuga matatizo makubwa kwani siku
nyingine akikukosea hata jambo dogo,
utakumbushia na ya jana na juzi na mwisho
ugomvi utakuwa mkubwa sana .
Tukutane wiki jayo kwa mwendelezo wa
mada hii nzuri . Kwa maoni , ushauri au swali
nicheki kwa namba za hapo juu .

No comments