SIFA 6 ZA MWANAUME ANAYESTAHILI KUWA MUMEO!


Wiki hii nitazungumzia sifa 6 za mwanaume
ambaye anastahili kuwa mumeo. Nafanya hivi
ikiwa ni msaada kwa wale ambao wamefikia
hatua ya kuingia kwenye ndoa lakini bado
wanashindwa kutambua yupi ni sahihi na yupi si
sahihi kuitwa mume.
Tufahamu kwamba si kila mwanaume
unayekutana naye na ukampenda anafaa kuwa
mumeo. Wengine wana mapungufu makubwa
ambayo bila kuyabaini na ukaingia
kichwakichwa, utakutana na matatizo makubwa.
Kwa maana hiyo basi, sifa hizi sita ambazo
nitazizungumzia leo endapo utaziona kwa huyo
ambaye macho yako yameganda kwake, fanya
maamuzi sahihi ya kumkubalia.
Anakupenda kwa maana ya kukupenda
Unapoingia kwenye maisha ya ndoa, unatarajia
kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwenza
wako. Wapo wanaume ambao wanaonesha wazi
kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na
mapenzi ya kuzuga.
Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu
kwamba yuko na demu flani bomba au kuonja tu
penzi kisha kuanza visa ili muachane.Kwa nini ni
vizuri kumpata mwanaume mwenye mapenzi ya
dhati? Hii inatokana na ukweli kwamba kinyume
na hivyo, maisha yatakuwa ya migogoro kila
siku. Atakufanyia mambo ya kukuumiza kwa
kukusaliti bila kujali maumivu utakayopata. Hii
yote ni kwa sababu hana mapenzi ya kweli na
wewe.
Ndiyo maana unashauriwa kwamba, kabla hata
ya kumuonjesha penzi kisha kufanya maamuzi
ya kumruhusu aende kwa wazazi wako ili
mfunge pingu za maisha, ni vyema ukawa na
uthibitisho kwamba anakupenda kwa moyo
mmoja.
Hili la tabia ndo’ kila kitu
Linapokuja suala la ndoa, tabia inakuwa kitu cha
awali sana kuangaliwa. Hii ni kwa sababu, wapo
wanaume ‘handsome’, wenye kazi nzuri na
kipato kizuri lakini wanakosa sifa ya kuitwa
mume kutokana na tabia zao chafu.
Hakuna mwanamke anayeweza kudiriki kumpa
nafasi mwanaume kuwa mume wake wakati ana
tabia chafu. Endapo utaangalia uzuri wa sura
kisha ukafanya maamuzi ya kuolewa naye,
utakuwa umejichimbia kaburi.
Awe anaota mafanikio
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina
yake kwa wanawake. Wengi hawapendi kabisa
kuolewa na mwanaume ambaye hana kazi.
Mwanaume anatakiwa kuwa dereva katika safari
ya kusaka mafanikio, sasa kama atakuwa ni mtu
wa kukaa kijiweni, kupiga mizinga, mvivu
asiyependa kujishughulisha kwa namna yoyote,
huyu hafai kupewa nafasi ya kuitwa mume.
Ile dhana ya kukubali kuolewa na mwanaume
yoyote ili mradi upate heshima ya kwamba
umeolewa, imepitwa na wakati. Mwanaume
sahihi ni yule mwenye malengo maishani,
anayefikiria nini cha kufanya kwa ajili ya
maendeleo yake, mkewe na watoto wao.
Wa shida na raha
Wapo wanaume ambao siyo wavumilivu kabisa
katika maisha.Tunajua maisha siku zote
hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya
kiafya ama kifedha.
Kwa mfano, unaweza kuingia kwenye maisha ya
ndoa lakini kwa bahati mbaya ukawa huna
kizazi, mwanaume mwenye mapenzi ya kweli na
wewe anatakiwa kukuvumilia na kuwa upande
wako.
Yule ambaye atakuwa anaungana na dada zake
kukushambulia kwa kutozaa, hafai kuwa na
wewe kwani yapo mengi yanayoweza kutokea
yanayohitaji kuvumiliana.
Kimsingi uvumilivu kwa mwanaume utakuwepo
kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama
nilivyozungumza hapo awali. Mwanaume
mwenye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa
mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika
maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya
starehe.
Anayejua thamani ya mke
Wapo wanaume ambao hawajui thamani ya mke
na ukiwachunguza utabaini hawafai kuwa waume
za watu. Mume sahihi ni yule anayejua kwamba
mke ni kitu cha faraja kwenye maisha yake.
Yule anayeamini kwamba, bila mke maisha yake
hayawezi kuwa yamekamilika. Wapo ambao
wanaamini hata bila wanawake wanaweza kuwa
na maisha mazuri.
Mwanaume mwenye dhana hii, ukimpa nafasi
kwenye moyo wako na ukaingia naye kwenye
maisha ya ndoa, lazima atakuwa mguu ndani,
mguu nje. Hataona hatari kukupa talaka hata
kwa jambo dogo tu ambalo mnaweza kuongea
na mkalimaliza.
Ndiyo maana nikasema, mwanaume sahihi wa
kumpa nafasi ya kuwa mumeo ni yule anayejua
thamani ya mke, anayeweza kuvumilia yote
akijua mke ndiye anayekamilisha maisha yake.
Asiye na tamaa za kijinga
Unaweza kuwa na mpenzi wa kawaida ukiwa na
malengo ya kumfanya awe mumeo katika siku
za baadaye. Huyu ukigundua ana tamaa, huna
sababu ya ‘kumpetipeti’.
Wanaume wenye tamaa za kijinga ndiyo ambao
wakishaingia kwenye maisha ya ndoa wanakuwa
wepesi kusaliti. Hao hawastahili kuitwa waume
za watu.
Mwisho kabisa naomba niseme kwamba, licha
ya sifa hizo 6, yapo mambo mengine ambayo
ukiyaona kwa mwanaume ambaye ulikuwa
unahisi anafaa kuwa mumeo, ni vyema
ukapingana na mawazo.
Mwanaume asiyepitwa na sketi, asiyependa
kumsikiliza mwenza wake, anayependa kufanya
maamuzi bila kutaka kumshirikisha mwenza
wake, anayekuwa upande wa ndugu zake
unapokuwa kwenye matatizo, asiyejali familia
yake, anayekuona wewe si lolote, asiyethamini
na kuwaheshimu ndugu na marafiki zako, huyo
kaa naye mbali kabisa.
Ni hayo kwa leo.

No comments