
MTAIPENDA hii kwani imekaa vizuri. Kocha mpya wa Simba, Goran
Kopunovic, ameshaanza kazi pale Msimbazi lakini straika wa Yanga, Danny
Mrwanda amewaambia wenzake: “Tulieni najua kila kitu chake, hawezi
kutusumbua.”
Kopunovic na Mrwanda walikutana Vietnam katika
klabu ya Dong Tam Long An na walifanya kazi pamoja kwa muda kidogo kabla
ya straika huyo kuhamia timu nyingine, Hoang Anh Gia Lai.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mrwanda alisema
amefurahi kukutana tena na kocha wake huyo wa zamani hata kama sasa wapo
timu tofauti na amemtaka bosi wake wa Yanga, Hans Van Der Pluijm na
wachezaji wenzake kutokuwa na wasiwasi kuhusu Kopunovic.
Mrwanda alisema Kopunovic ni kocha mzuri na siku
zote amekuwa anapenda kuona kikosi chake kikitengeneza mashambulizi
makali kupitia viungo wa pembeni ambao huwaagiza kupiga krosi za kutosha
kwa washambuliaji wa kati.
Straika huyo ambaye amewahi kuichezea Simba,
alisema Kopunovic mbali na hilo anapenda kuona kikosi chake
kikishambulia kwa kasi huku mashambulizi yakianzia kwa mabeki ambao
hawatakiwi kukaa na mpira muda mwingi na kutakiwa kuuachia haraka kwa
viungo au mabeki wa pembeni ambao nao jukumu lao ni kuwatafuta viungo wa
pembeni yaani mawinga.
“Unajua mimi sioni kama kuna hatari katika timu
yetu kuhusu ujio wa Goran (Kopunovic), tuna timu ambayo inaweza
kupambana kutokana na uzoefu na kocha mwenye uwezo mkubwa wa kuwasoma
wapinzani wake,” alisema Mrwanda.
“Nitamweleza Pluijm kuwa siku zote Kopunovic ni
kocha anayependa timu yake kutumia mawinga na hata viungo wa kati
kutengeneza mashambulizi sasa mkikutana na timu yake na mkafanikiwa
kuwabana katika maeneo hayo uwezekano wa kumshinda mnao.
“Tulivyokuwa naye alikuwa anawazuia kabisa mabeki
kukaa na mpira amekuwa akitaka wauachie haraka na kuwapa aidha mabeki wa
pembeni au viungo wa kati ambao nao jukumu lao ni kupeleka mbele kwa
mawinga, soka analopenda ni la kasi kidogo,” alisema Mrwanda.
Kopunovic aliyesaini mkataba wa miezi sita,
alitarajiwa kuanza kazi jana Alhamisi kwa kuiongoza Simba katika mchezo
wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan,
Zanzibar
Post a Comment