Jinsi Phiri alivyoondolewa kiaina na kumpa Mserbia miezi 6



KWELI mambo ni kizungumkuti kwani Simba imempa mkataba wa miezi sita Kocha Goran Kopunovic na hapo hapo imempa ‘likizo’ Patrick Phiri aende kwao Zambia akapumzike.
Kopunovic raia wa Serbia amekubali kusaini mkataba huo ambapo analipwa dola 3000 kwa mwezi (Sh5 milioni) wakati Phiri alikuwa analipwa dola 2000 (Sh3.3 milioni) tofauti kati yao ikiwa ni dola 1000 (Sh1.7 milioni).
Phiri amesitishiwa mkataba wake ‘kiaina’ baada ya timu hiyo kutokuwa na matokeo mazuri katika mechi nane za Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya kumi na pointi zake tisa. Simba imetoka sare sita, imeshinda mechi moja na kufungwa mara moja.
Kwa siri uongozi wa Simba ukafanya mazungumzo haraka na Kopunovic ili aje kuinusuru timu yao ambao kocha huyo aliwasili nchini juzi Jumatano asubuhi kisha kufanya mazungumzo na matajiri wa timu hiyo ambao jana walimpa mkataba wa miezi sita.
Kocha alitarajiwa kwenda Zanzibar muda wowote baada ya kusaini mkataba huo kuiongoza Simba dhidi ya Mtibwa Sugar katika Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan.
Kopunovic amekubali kufanya kazi hiyo kwa mshahara huo unaoonekana kiduchu baada ya kujiridhisha na mazingira ya timu anayojiunga nayo. Aliyekuwa Kocha wa Simba, Mserbia Dravko Logarusic alikuwa analipwa dola 5000 (Sh8 milioni).
“Unajua Waserbia huwa hawachukui fedha nyingi sana, lakini hii yote inategemea na makubaliano ya fedha wakati wa kusaini mkataba, Phiri alichukuwa fedha nyingi katika kusaini mkataba kuliko huyu ndiyo maana mishahara ipo tofauti,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba.
FIDIA YA PHIRI
Ni wazi Simba sasa inamtafuta mtu maalumu wa kumpasulia ukweli Phiri kwamba hawatakuwa naye tena, lakini klabu hiyo italazimika kumlipa kocha huyo dola 8000 (Sh13.5 milioni) za fidia na malipo ya mishahara yake ya miezi mitatu ambayo hakulipwa.
Kwa mujibu wa mkataba wa Phiri na Simba, yeyote atakayevunja mkataba anatakiwa kumlipa mwenzake mshahara wa mwezi mmoja. Akizungumza na Mwanaspoti, Phiri alisema; “Maisha ya soka ndivyo yalivyo na unatakiwa kujiandaa kwa lolote na muda wowote, wamemleta kocha bila kuniambia lolote na nilipowauliza kuhusu hali hiyo wamekataa, ndiyo maana nimewaambia niende nyumbani kwa mapumziko mafupi na wamekubali.
“Mambo ya kufukuza kocha siyo ya kufichana kwani mimi siyo lazima niifundishe Simba, Aveva (Evan, Rais wa Simba) ni rafiki yangu na ndiye alinipigia simu nikiwa Zambia kuniomba nije hapa iweje sasa ashindwe kuniambia kama alivyofanya hapo awali.
“Naamini haki zangu watanilipa na hata kama wakiamua kutonilipa nitahesabia kama nimepoteza kwa bahati mbaya, pia nitamshukuru Mungu,” alisema Phiri. “Nitaondoka kesho (leo) labda nikifika Zambia au wakati wa kuondoka ndiyo nitaambiwa rasmi, ila namtakia kila la kheri kocha mpya aiwezeshe Simba kupata matokeo mazuri.”

No comments