
WINGA wa Yanga, Simon Msuva ameifungia timu yake mabao matatu
‘hat trick’ kisha akatoa pasi ya bao la nne na kuiwezesha kuibuka na
ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Taifa Jang’ombe jana usiku kwenye Uwanja
wa Amaan, Zanzibar.
Nyota ya Msuva ilianza kuonekana mapema kutokana
na kuwazidi kasi mabeki wa Taifa Jang’ombe mara kwa mara akicheza kwa
ushirikiano na straika Kpah Sherman.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alibadilisha
kikosi cha timu yake na kuwajumuhisha kwenye kikosi cha kwanza wachezaji
Ally Mustapha ‘Bathez’, Pato Ngonyani na Mrisho Ngassa ambao hawakuwa
wakipata nafasi hiyo mara kwa mara.
Msuva aliipatia Yanga bao la kwanza dakika ya 13
akimalizia mpira uliotemwa na kipa Kasim Mussa aliyekuwa katika harakati
za kuokoa shuti la Sherman. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Msuva aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 49 akiunganisha pasi ndefu ya Telela.
Winga huyo mwenye kasi alifunga tena dakika ya 64 akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Andrey Coutinho.
Wakati mashabiki wakidhani Yanga ingepata ushindi
wa mabao 3-0, Msuva alipiga krosi safi iliyomfikia Sherman ambaye
aliifungia timu yake bao la nne dakika ya 90.
Kwenye mchezo huo Yanga ilicheza vizuri ndani ya
dakika 20 za kwanza kabla ya kupotea lakini ilirejea kipindi cha pili
ikiwa na kasi iliyowasaidia kupata mabao manne.
Taifa Jang’ombe ilionekana kukosa uzoefu wa
kupambana na timu yenye kasi kama Yanga. Straika wa Yanga, Hussein Javu
alikimbizwa hospitalini baada ya kugongana na beki wa Taifa Jang’ombe
wakati Msuva alizawadiwa mpira wake baada ya kufunga ‘hat trick’ hiyo.
Katika mechi za awali jana Ijumaa, Azam ilitoka sare ya mabao 2-2 na
KCCA huku KMKM ikitoka suluhu na Mtende FC.
Kutokana na mabadiliko ya ratiba yaliyotangazwa jana usiku, Simba itacheza leo na Mafunzo ya Zanzibar uwanjani hapo.
Yanga: Ally Mustapha ‘Bathez’, Juma Abdul,
Pato Ngonyani, Oscar Joshua/Edward Manyama, Cannavaro, Telela, Msuva,
Hassan Dilunga/Haruna Niyonzima, Sherman, Mrisho Ngassa/Amissi Tambwe,
Coutinho/Hussein Javu.
Taifa: Musa, Omar Chande, Hafidh Bakari, Abdallah
Shaibu, Abrahaman Abdallah, Khamis Khamis, Abdallah Mudathir, Abdul
Seif, Hafidh Barik,Nabil Juma, Bahati Bahanuzi.
Post a Comment