
KOCHA mpya wa Simba, Goran Kopunovic
ameanza kazi ya kukinoa kikosi cha timu yake visiwani Zanzibar huku
akitakiwa kuwa makini na msimamo juu ya usumbufu wa mshambuliaji
Emmanuel Okwi vinginevyo ataharibikiwa mapema tu.
Aliyetamka maneno hayo si mwingine bali ni Patrick
Phiri kocha aliyesitishiwa mkataba wake na kuondoka nchini jana Ijumaa
asubuhi kurudi kwao Zambia ambaye amemtakia kila la kheri Kopunovic
katika kazi yake.
Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu
yaliyofanyika saa chache kabla ya kuondoka kwake, Phiri alisema kuwa
katika kikosi cha Simba alichokaa nacho kwa miezi mitano hakuna mchezaji
msumbufu kama Okwi lakini viongozi wanafumbia macho usumbufu wake.
“Okwi ni msumbufu sana na huyu kocha mpya (Goran)
kama atakuwa mpole atamsumbua sana, sijawahi kuona mchezaji wa kimataifa
msumbufu kama Okwi akienda kwao anarudi siku moja au mbili kabla ya
mechi na viongozi hawasemi lolote.
“Kocha asikubali tabia hii ya Okwi iendelee ndani
ya timu, binafsi sijakaa naye muda mwingi lakini ndiyo hivyo huwezi
kusema lolote kwa viongozi juu ya Okwi wakakuelewa, Okwi ni mchezaji
mzuri sana ila tabia zake kama hizi ndizo zinazokera na zitamrudisha
nyuma,” alisema Phiri.
Phiri alimtaka mchezaji huyo kulinda kipaji chake kwa kujituma na kuwa na nidhamu ndani ya timu.
“Nidhamu haifundishwi na mtu ni jinsi mtu mwenyewe
anavyoishi na kutaka kuwa hivyo, Okwi ana kipaji kikubwa lakini anaweza
kukishusha mwenyewe kwa tabia zake, namshauri atulie acheze mpira
atafanikiwa zaidi kwani Simba wanampa kila kitu afanye kazi
iliyomleta,”.
Kwa sasa Okwi ameaga kwenda kwao Uganda kumalizia
fungate baada ya kufunga ndoa hivi karibuni, lakini hadi juzi Alhamisi
jioni alikuwepo Dar es Salaam. Mchezaji huyo ana ruhusa hiyo wakati timu
ipo visiwani Zanzibar inakoshiriki Kombe la Mapinduzi.
Post a Comment