Simba noma! Yachezea akili za Yanga, Azam



SIMBA ni kama inacheza na akili za Yanga na Azam baada ya kumsafirisha kocha wake, Dylan Kerr kutoka visiwani Zanzibar kuja kutazama mechi ya robo fainali ya Kombe la Kagame baina ya timu hizo juzi Jumatano ambapo Yanga ililala penalti 5-3.
Jitihada hizo za Simba ni kuhakikisha kuwa kocha huyo anapata kuzisoma vizuri timu hizo ambazo zinatarajiwa kumpa wakati mgumu katika mbio za ubingwa Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Hata hivyo, licha ya kutumia dakika zote 90 kuzifanyia tathmini timu hizo, Kerr alisema mechi ya juzi ilikuwa na changamoto zake na ni ngumu kubaini uwezo halisi wa timu hizo kwani zote ziliingia uwanjani kwa kujihami zaidi kuliko kucheza soka lao walilolizoea.
Kocha huyo Mwingereza aliyepewa mkataba wa kuifundisha Simba kwa miaka miwili, aliongeza kuwa Azam ilikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kumaliza mchezo huo mapema kutokana na kuwa na safu imara ya ulinzi na pia kupata nafasi nyingi za wazi zaidi ya Yanga.
Azam ilitinga hatua ya nusu fainali kwa changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare tasa.
Hata hivyo Kerr alibainisha kuwa Ligi Kuu itakuwa ngumu kuliko michuano ya Kagame na ndipo uwezo halisi wa Yanga na Azam utaonekana vizuri kuliko ilivyokuwa hapo juzi.
“Timu zote ziliingia kwa kujihami, hakuna aliyekuwa tayari kupoteza mchezo, kwa upande wangu nadhani Azam walikuwa na nafasi ya kumaliza mchezo mapema kutokana na kupata nafasi nyingi za wazi ambazo walishindwa kuzifanyia kazi,” alisema Kerr.
“Unapokuwa na safu nzuri ya ulinzi unakuwa na uhakika wa ushindi, mechi nne kwa Azam bila kuruhusu bao ni kiwango cha juu, ningependa timu yangu iwe na rekodi kama hizo.
“Kuhusu uwezo wa Yanga na Azam wapinzani wangu katika ligi siwezi kusema sana, katika mashindano mafupi ni vigumu kufahamu uwezo halisi wa timu, ligi ndiyo kila kitu, hapo tutabaini uwezo wao.”

No comments