Marais watano wanaotajwa kuongoza kwa mishahara minono barani Afrika hawa hapa

Wakati Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akiupunguza mshahara wake muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka huu, marais wengine wa  Afrika wameonekana kujilimbikizia mishahara mikubwa, tofauti na pato  ‘kiduchu’ la wananchi wao kwa mwaka.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa mtandao wa African Review, marais watano wanaoongoza kwa kuwa na mishahara mikubwa kwa mwaka ni  Rais Paul Biya wa Cameroon anayelipwa Dola za Marekani 610,000, akifuatiwa na kiongozi wa Morocco, Mfalme Mohammed VI anayelipwa Dola 480,000 na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ni wa tatu akilipwa Dola 272,000.
Rais Jakaya Kikwete ni wa nne kwa malipo ya Dola 192,000 na wa tano ni Rais Abdel Aziz Bouteflika wa Algeria, anayelipwa Dola168,000.
 Mtandao huo umebainisha pato la Mtanzania wa kawaida kwa mwaka kuwa ni Dola 1750 sawa na Sh3.5 milioni, linalozidiwa mara 114 na kiasi anacholipwa Rais kwa mwaka.
Madhumuni ya utafiti wa mtandao huo ilikuwa kuangalia kiasi wanacholipwa marais wa Afrika kwa mwaka na  kile inachopata taifa husika kwa muda huo.
Pia walilenga kuangalia  uhusiano wa viongozi hao na wananchi  wa kawaida wanaowangoza.
Kwa  mujibu wa mtandao huo, vyanzo  vya taarifa za mishahara ya marais hao vilipatikana kutoka mitandao na wanahabari wa nchi husika.
 Tofauti na maraisi wengine, Rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari,  alitangaza punguzo la mshahara wa rais pamoja na wafanyakazi wengine  wa Serikali mara alipoingia madarakani.
 Rais mwingine aliyefanya hivyo ni Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambaye pamoja na makamu wake walipunguza mishahara yao kwa asilimia 20 baada ya kuingia madarakani mwaka 2013.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo marais wa nchi zilizoendelea bado wanapata mshahara mkubwa, ingawa  unaendana na kipato cha mwananchi wa kawaida kwa mwaka.
Kwa mfano, Rais Barack Obama wa Marekani anapata mshahara wa Dola 400,000 kwa mwaka.  Stephern Harper wa Canada, Dola 260,000 na Angela Merkel wa  Ujerumani, Dola 234,000.
 Rais wa zamani wa Tunisia, Moncef Marzouk,  baada ya kukumbwa na mgogoro wa kiuchumi, alitangaza punguzo la robo tatu ya mshahara wake kwa mwaka kutoka Dola 176, 868 hadi  Dola 58,956. 
 Kitendo cha Rais Marzouk, Buhari na Kenyatta kimeonekana  ni tofauti na marais wengine ambao huongeza mishahara yao baada ya kuingia madarakani.
Kwa mfano, Rais wa Misri alijiongezea mshahara kutoka Dola 280 kwa mwezi, kiwango ambacho kiliwekwa na rais wa awali Mohammed Morsy hadi Dola 5,900 kwa mwezi.
 Hata hivyo katika nchi nyingine, viongozi huchukua pato la nchi kwa ajili ya matumizi yao binafsi. Kwa mfano nchini Morocco, Dola 1 milioni hutumika kwa siku kwa ajili ya makazi  12 ya kifalme ya Mfalme Mohammed VI na makazi yake mengine binafsi 30.
Wakati huo, Dola7.7 milioni  hutumika kwa ajili ya magari ya kifalme na  Dola 40,000 kwa ajili ya mshahara wa mwezi kwa wafanyakazi wa makazi ya kifalme.
 Mwaka 2014, Mfalme Mswati wa Swaziland, alijiongezea bajeti yake, ambayo inajumuisha mshahara na wanafamilia wake kwa asilimia 10.  Aliongeza Dola 61 milioni kwa kunyofoa kiwango kikubwa cha bajeti kuu ya Serikali yake ya kifalme. 
Hata hivyo, kulingana na masharti ya nchi za kifalme,  ongezeko hilo huwa halijadiliwi  bali huwa sheria moja kwa moja.
 Marais wengine hujitengea mishahara midogo machoni mwa umma, lakini wanafamilia wao humiliki biashara au kampuni nyingi.  Kwa mfano,  Rais Eduardo dos Santos wa  Angola, anapokea mshahara wa Dola 5,000 lakini anaaminika kumiliki kiasi kikubwa cha utajiri kwenye viwanda vya mafuta, huku wanafamilia wake pia wakimiliki viwanda hivyo.
Katika nchi ya Guinea Equator, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na  idadi ya watu chini ya milioni moja, bado nchi hiyo inatajwa kuwa na pato la juu la nchi. Hata hivyo kiasi kikubwa cha utajiri huo kinamilikiwa na watu wachache na familia ya rais.
 Kitengo cha Sheria cha Marekani kilimshtaki mtoto wa  kwanza wa Rais wa Equatorial Guinnea, Teodoro Nguema Obiang Mangue, kwa  kutumia Dola 315 milioni kununua nyumba na  bidhaa nyingine za kifahari kati ya mwaka 2004 na 2011, licha ya kuwa ni waziri wa nchi hiyo anayelipwa chini ya Dola 100,000 kwa mwaka.
 Uchambuzi wa Africa Review ulipochambua tena mishahara ya viongozi hao kwa kuulinganisha na pato la nchi kwa mwaka, bado  marais Paul Biya wa Cameroon,  Ellen Johnson Sirleaf wa Nigeria, Jakaya Kikwete, Peter Mutharika wa Malawi na Joseph Kabila wa Congo walibainika ndiyo wanaolipwa mara 100 zaidi ya mapato ya mataifa yao kwa mwaka.

No comments