Mambo ni shwari Yanga



LICHA ya kupoteza penalti mbili kwa mpigo katika kipindi cha kwanza, Yanga jana Jumatano ilifanikiwa kufufua matumaini yake katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuicharaza Telecoms ya Djibout mabao 3-0.
Utamu ulikuwa kwa winga mpya ya Yanga aliyeingia kipindi cha pili, Geofrey Mwashiuya, kwa jinsi alivyofanya yake kukoleza ushindi huo.
Mchezaji huyo mpya kikosini humo alikuwa chachu kubwa kwa mashambulizi aliyoyajenga.
Mwashiuya aliifungia Yanga bao la tatu kwa shuti la umbali wa mita 25 baada ya kuwapunguza mabeki wawili wa Telecoms, ambapo kombora lake liligonga mwamba kisha kumgonga kipa Nzokira Jeef na kutinga wavuni.
Katika pambano hilo la Kundi A lililochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, wana Jangwani hao walipoteza penalti hizo kwa mpigo kupitia nyota wake waliongoza orodha ya wafungaji Bora wa Ligi Kuu Bara uliopita; Amissi Tambwe na Simon Msuva.
Penalti hizo ziliotolewa na mwamuzi Issa Kagabo kutoka Rwanda katika dakika za 38 na 45 baada ya mabeki wa Telecoms kufanya madhambi langoni mwao.
Hata hivyo Yanga haikunufaika nazo kwani zilipotezwa na kuifanya iwe imepoteza penalti tatu mfululizo baada ya awali Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kukosa dhidi ya Gor Mahia katika mechi ya fungua dimba Jumamosi iliyopita pia uwanjani hapo.
Jana Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kukosa mabao mengi ya wazi kabla ya Malimi Busungu kuiandikia bao la kuongoza katika dakika ya 26 akiunganisha kwa shuti kali krosi kutoka kwa beki wa kulia Joseph Zuttah aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
Telecoms ilionyesha upinzani ikikosa mabao ya wazi kabla ya kuruhusu bao la Busungu, huku penalti mbili zilizokoswa ambazo hata hivyo walizilalamikia wakihisi kuonewa na refa ziliwafanya wapoteze umakini zaidi na kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Tambwe na Msuva na kuwaingiza Kpah Sherman na Mwashiuya walioiongezea uhai safu ya mbele ya Yanga ambapo katika dakika ya 66 iliandika bao la pili kupitia kwa Busungu tena aliyemalizia kazi nzuri ya Mwashiuya.

No comments