Okwi aanzisha operesheni maalumu Msimbazi
KOCHA wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic na kipa wake, Ivo
Mapunda, wamempigia saluti straika wao, Emmanuel Okwi raia wa Uganda
ambaye ndani ya dakika 180 za michezo miwili waliyocheza, amekuwa
akifunga mabao ya staili moja kwa umbali wa zaidi ya mita 30 pembeni mwa
uwanja.
Lakini Okwi amesisitiza kwamba sasa wachezaji
wameanzisha operesheni maalum ambayo ubingwa haupo akili mwao kabisa,
wanapiga moja moja baadaye kitaeleweka tu.
“Tunaweka kando suala la ubingwa na tunachotakiwa kufanya ni kushinda kila mechi halafu baadaye ndiyo itajulikana,” alisema.
Mganda huyo ameongeza kusema huwa hakosei kwa
sababu amekuwa akiyafanyia kazi mara kwa mara anapokuwa mazoezini. Okwi
amefunga mabao hayo mfululizo kwenye mechi yao na Yanga waliyoshinda 1-0
alifunga umbali wa mita 30 na juzi Jumamosi aliwafunga Mtibwa bao 1-0
umbali wa mita 35.
Mabao ambayo yamewapa raha mashabiki wa Simba
ambao baada ya mechi, wamekuwa wakikusanyika nje ya uwanja na kuiimba
“Okwi, Okwi.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Okwi alisema: “Nimekuwa
nafunga mabao ya aina hiyo kwa sababu huwa ninayafanyia kazi mara
nyingi ninapokuwa mazoezini ndiyo maana inakuwa rahisi kwangu kufunga.
Kama hili la Mtibwa, dakika zilivyokuwa zimekwisha, wakajua mechi
imemalizika wakajisahau, mimi nikamwangalia kipa alivyokaa nikafunga.”
Okwi ambaye alitoka uwanjani Jumamosi akiwa amejaa
noti alizozawadiwa na mashabiki, aliongeza: “Lakini kingine mbali na
mazoezi, wachezaji ninaocheza nao, wananipa ushirikiano mzuri na ndiyo
maana tunafanikiwa.”
Golan alisema ana kila sababu ya kumsifu Okwi
kutokana na kiwango chake anachokionyesha uwanjani. Okwi aliwafunga
Yanga kipa akiwa Ally Mustapha ‘Barthez’ na alipowafunga Mtibwa, mlinda
mlango alikuwa, Said Mohamed. Mabao hayo yamewaweka matatani makipa hao.
Post a Comment