Mkakati wa CCM kumfukuza Lowassa uanachama huu hapa
MBUNGE wa Monduli, Edward Ngoyai Lowassa, aweza kuvuliwa uwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), muda wowote kutoka sasa. Saed Kubenea, anaripoti.
Hoja ya kumvua uanachama Lowassa imepangwa kuwasilishwa
katika kikao cha Kamati Kuu (CC), kinachotarajiwa kufanyika Jumanne wiki
hii, mjini Zanzibar.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, mkakati wa kumvua uwanachama Lowassa, unasukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya viongozi wandamizi ndani ya CCM ili kumzua kutimiza ndoto yake ya kuwa rais.
“Ni lazima tumfukuze uanachama katika chama chetu. Hakuna
namna nyingine ya kukinusuru chama hiki,” ameeleza kiongozi mmoja
mwandamizi ndani ya chama hicho.
Amesema, “Bwana huyu (Lowassa), amekuwa akikivuruga chama
chetu kwa muda mrefu. Tumemvulia, lakini sasa tumechoka. Nilazima
tumuondoe ili kukinusuru chama chetu.”
Ajenda ya kumfukuza Lowassa kutoka ndani ya chama hicho,
imejificha katika kinachoitwa, “Tathmini hali ya kisasa kuelekea
uchaguzi mkuu wa mwaka huu.”
Lowassa alikuwa waziri mkuu wa kwanza katika serikali ya
Jakaya Kikwete. Anatajwa kuwa miongoni mwa makumi ya wanachama wa CCM
waliotangaza au kutajwa, kusaka urais kwa udi na uvumba katika uchaguzi
mkuu ujao.
Januari mwaka jana, Lowassa na makada wenzake kadhaa
walipewa “onyo” kwa kile kilichoitwa, “kuanza kampeni kabla ya muda
kufika.”
Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema, kabla ya kikao cha
CC, kutafanyika kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili na Nidhamu, ambacho
kitafanya tathmini ya adhabu zilitolewa kwa Lowassa na wenzake.
Lowassa anatuhumiwa kuendelea na mkakati wake wa kampeni
kwa kukusanya watu na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, jambo
ambalo viongozi wake wakuu wanamtuhumu kukipasua chama chao.
Anasema, kikao cha CC kitatekeleza mradi huo kwa kutumia
ripoti zilizotengenezwa na timu za maofisa usalama wa chama hicho,
zilizotumwa mikoa yote ili kukusanya kile kilichoitwa, “mkakati wa
Lowassa wa kusaka urais.”
Kutokana na hali hiyo, Kamati Kuu iliitaka Kamati ya
Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada
hao sita.
Mtoa taarifa anasema, baada ya kikao cha Kamati ya Maadili
kumalizika, kutawasilishwa kwa Rais Kikwete pendekezo la kumfukuza
Lowassa kutoka katika chama hicho.
Mkutano wa Kamati Ndogo ya Maadili, utakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kuna
uwezekano mdogo mno kwa Kikwete kuweza kusimamia mradi huo hadi mwisho.
“Pamoja na mkakati huo kuendeshwa na viongozi wajuu wa
CCM, lakini bado uwezekano wa kuutekeleza unakuwa mgumu. Hii ni kutokana
na mwenyekiti Kikwete kuwa kigeugeu,” anaeleza kiongozi mmoja
mwandamizi wa chama hicho
Post a Comment