Tambwe aiduwaza CAF
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe amefanikiwa kucheza mechi ya kwanza ya mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ndani ya ardhi ya Tanzania.
Katika hilo Tambwe pia amefanikiwa kuweka rekodi
moja ya awali katika soka la Afrika, rekodi ambayo itaendelea kuwa
katika kumbukumbu za CAF.
Yanga ambayo inashiriki mashindano ya Kombe la
Shirikisho Afrika, wikiendi iliyopita ilivuna ushindi wa kwanza wa mabao
2-0 dhidi ya BDF XI ya Botswana yote yakifungwa na Tambwe.
Katika mechi 23 za Kombe la Shirikisho
zilizochezwa katika siku mbili za Februari 14 na 15, jumla ya mabao 43
yalifungwa katika mechi hizo lakini mabao mawili pekee ndiyo yameweka
rekodi ya kufungwa mapema zaidi yakifungwa na timu mbili kutoka Afrika
Mashariki.
Rekodi ambayo Tambwe amefanikiwa kuiweka Afrika ni
juu ya bao la mapema ambapo mpaka mechi za kombe hili zikikamilika jana
alikuwa yeye na kiungo mwingine wa Afrika Mashariki wakifunga mabao
hayo ya mapema.
Tambwe aliifungia Yanga bao dakika ya kwanza ya mchezo huo dhidi ya BDF XI kwa kichwa akipokea krosi ya kiungo Haruna Niyonzima.
Mbali na Tambwe kiungo wa Rayon Sport ya Rwanda
Leon Uwambazimana amefanikiwa kufungana na Tambwe baada ya kufanikiwa
kuifungia timu hiyo yenye mashabiki wengi Rwanda bao hilo pekee katika
dakika ya kwanza wakati walipoumana na Panthere ya Cameroon.
Achana na hilo, Tambwe, mshambuliaji mtulivu
kutoka Burundi aliyevuna Dola 20,000 (Sh34 milioni) katika usajili wake
akitokea Simba, mpaka sasa amefanikiwa kuweka rekodi nyingine katika
kikosi cha Yanga baada ya kuzifunga timu mbili tofauti mabao manne yote
akitumia kichwa.
Ipo hivi; Tambwe mpaka anaondoka Simba katika nusu
ya mzunguko wa kwanza alifanikiwa kuifungia timu hiyo bao moja pekee
dhidi ya Coastal Union akitumia krosi ya Emmanuel Okwi wakati timu hizo
zikitoka sare ya mabao 1-1.
Akiwa Yanga Tambwe amefanikiwa kufunga mabao
matatu moja akifunga dhidi ya Azam katika Ligi Kuu Bara ukiwa mchezo
wake wa kwanza tangu asajiliwe akifunga kwa kichwa akitumia krosi ya
kiungo mkabaji, Salum Telela.
Kama haitoshi Februari 14 Jumamosi iliyopita
alifungua ukurasa wake wa mabao ya Kimataifa ndani ya timu hiyo
akiyafunga kwa kichwa akitumia krosi za Niyonzima na winga Mrisho Ngassa
na hivyo kulitangaza jina lake Afrika kwa rekodi hiyo.
Post a Comment