Yanga yamshtukia mpelelezi.. Soma hapa


INAONEKANA timu zimeamka na kuweka utaifa mbele, kwani Yanga imemnyima taarifa muhimu Kocha Msaidizi wa El Merreikh, Burhan Tia (pichani), aliyetua Zanzibar kwa lengo la kuichunguza Azam FC watakayokutana nayo mwezi ujao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
El Merreikh ya Sudan imemtuma Burhan visiwani hapa ili atazame mbinu za Azam inayoshiriki Kombe la Mapinduzi na ili kupata urahisi wa kazi yake, kocha huyo alifikia katika hoteli moja ilipo kambi ya Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Burhan alisema kazi yake imekuwa ngumu kwani baada ya kuwaomba Yanga msaada wa kumpa siri muhimu kuhusu Azam, viongozi wa timu hiyo wamegoma kumpa ushirikiano wowote wa maana.
Burhan alisema kabla ya kufika Zanzibar, aliambiwa kwamba Yanga haina uhusiano mzuri na Azam hivyo itakuwa rahisi kwake kuwatumia viongozi wake kupata taarifa muhimu za wapinzani wao kitu ambacho kimekuwa tofauti na alivyoelezwa.
“Nimeshangazwa kwa nini Yanga wamekataa, wamenikatalia kunieleza baadhi ya mambo ya Azam wakisema hawawezi kufanya hivyo kwani ipo siku na wao wanaweza kufanyiwa hivyo na Azam na pili wanatazama utaifa kwani Azam inawakilisha Tanzania,” alisema.
“Hata hivyo nashukuru nimeweza kwenda uwanjani na kuitazama Azam ikicheza na kushinda bao 1-0 (dhidi ya KMKM) hivyo ninavyo vitu vya kuanzia licha ya Yanga kunikatalia kunieleza mambo mengine.
“Unajua Azam tulicheza nayo Rwanda lakini tumeambiwa kwamba kikosi chao kina mabadiliko makubwa tukaona ni vizuri tuitazame tena kujua ilivyobadilika, naendelea kuifuatilia.”

No comments