Yanga yaifumua Polisi.. Soma hapa
HATUREMBI! Hii ndiyo kauli ya Yanga jana Jumapili baada ya
kuendeleza ushindi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga
Polisi Zanzibar mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Amaan.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Yanga ambayo
katika mechi yake ya kwanza Ijumaa iliyopita iliifunga Taifa Jang’ombe
mabao 4-0 na sasa inaongoza Kundi A ikiwa na pointi sita na mabao
manane, haijafungwa hata bao moja.
Katika mchezo wa jana, Polisi ilionekana kucheza
vizuri dakika 20 za kwanza lakini haikuweza kuhimili kasi ya Yanga na
kujikuta ikiruhusu bao dakika ya 27 lililofungwa na Andrey Coutinho raia
wa Brazil. Coutinho alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira uliorushwa
na beki Oscar Joshua.
Straika wa Yanga, raia wa Liberia Kpah Sherman
aliifungia timu yake bao la pili dakika ya 33 akimalizia pasi safi ya
kichwa ya Amissi Tambwe.
Bao hilo liloonekana kuwa jepesi baada ya kipa wa
Polisi, Omar Mzee kushindwa kuokoa shuti hilo hafifu la Sherman. Mabao
hayo yalidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Yanga iliendeleza kasi yake na
kufanikiwa kupata bao la tatu kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Coutinho
dakika ya 56 baada ya straika Mrundi Amissi Tambwe kuangushwa nje kidogo
ya eneo la hatari.
Kwenye mchezo huo Coutinho alikuwa mwiba kwa mabeki wa Polisi ambao kila mara aliwazidi ujanja.
Licha ya Polisi kujitahidi kucheza kwa uangalifu
na kutumia nguvu, Yanga iliendelea na kasi yake na winga Simon Msuva
aliipatia bao la nne dakika ya 80 akimalizia pasi ya kiungo Salum
Telela.
Bao hilo limemfanya Msuva kufunga mabao manne
katika michuano hiyo baada ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ katika
mchezo dhidi ya Taifa Jang’ombe.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alisema:
“Nafurahi tumeshinda mabao mengi lakini bado sijaridhika na kiwango cha
washambuliaji, wanapoteza nafasi nyingi jambo ambalo linaweza
kutugharimu huko baadaye”
Kwa upande wake, Kocha wa Polisi, Hamis Sufiani,
alisema: “Nasikitika kwa matokeo haya, mipango yetu yote imefeli lakini
tutapambana mechi ya mwisho kuhakikisha tunasonga mbele.”
Yanga; Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar
Joshua, Cannavaro/Rajab Zahir, Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon
Msuva, Nizar Khalfan/Hassan Dilunga, Amissi Tambwe, Kpah Sherman/Danny
Mrwanda, Andrey Coutinho/Mrisho Ngassa.
Post a Comment